Baada ya suala la deni la taifa kuibua mjadala wakati hotuba ya bajeti ya Wizara ya Fedha na Mipango ikijadiliwa bungeni Dodoma, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji ametangaza kuwa Tanzania itafanyiwa tathmini ya deni hilo mwakani ili liweze kufahamika na watu wa ndani na nje ya nchi.
Dk. Kijaji ameeleza kuwa hadi kufikia Aprili 30 mwaka huu, Deni la Taifa lilikuwa Sh. 59.5 trilioni (takribani Dola za Marekani 26.16 milioni) ambapo deni hilo linajumuisha deni la serikali pamoja na lile la sekta binafsi. Naibu waziri huyo pia amesisitiza kuwa, serikali ina wajibu wa kulipa deni la serikali pekee na sio deni la taifa kwa ujumla.
Dk. Kijaji pia amewaeleza wabunge kuwa, serikali ilitenga kiasi cha Sh. 1.3 trilioni kwa mwaka wa fedha 2017/2018 maalum kwa ajili ya malipo ya deni la ndani na kiasi cha Sh.685.06 bilioni kwa ajili ya malipo ya deni la nje. Amesisitiza kuwa serikali inaendelea kukopa na kuaminiwa kwa sababu deni la taifa bado ni himilivu.