Na Mwandishi wetu
Thamani ya hisa katika Soko la Hisa la Dar es salaam (DSE) imepungua na kufikia Sh. 6 bilioni wiki hii kutoka Sh. 7.5 bilioni ya wiki iliyopita, huku hisa zilizouzwa na kununuliwa zikishuka kutoka hisa milioni 31 mpaka kufikia hisa laki nane. Akiongea na waandishi wa habari, Ofisa Mwandamizi wa Masoko wa DSE Mary Kinabo amesema licha ya kushuka kwa mauzo ya hisa, ukubwa wa mtaji wa kampuni katika soko umeongezeka.
Kinabo amedai kuwa mtaji wa kampuni ambazo zimeorodheshwa katika soko umeongezeka hadi kufikia Sh. 20.9 trilioni kutoka Sh. 20.6 trilioni ya wiki iliyopita kutokana na kupanda kwa bei ya hisa za Acacia (12%), NMG (10%), KA (9%), DSE (3%) na TBL (2%) hivyo kupelekea mtaji kuongezeka kwa Sh. 357 bilioni.
Katika kampuni za ndani, mtaji umeongezeka kwa Sh. 89 bilioni hivyo kufikia Sh. 9.9 trilioni kutoka Sh. 9.7 trilioni kutokana na ongezeko la bei ya hisa za DSE kwa asilimia tatu na TBL kwa asilimia mbili. Vilevile mauzo ya hati fungani yaliongezeka kutoka Sh. 192 milioni hadi Sh. 5.7 bilioni kutokana na hati fungani sita za serikali zenye thamani ya Sh. 6.5 bilioni kwa gharama ya Sh. 5.7 bilioni.