Home FEDHA Huduma ya Visa kupitia simu za mikononi yazinduliwa

Huduma ya Visa kupitia simu za mikononi yazinduliwa

0 comment 106 views

Kampuni ya VISA kwa kushirikiana na benki zipatazo 15 hapa nchini wamezindua huduma ya kwanza ya malipo ya simu bure. Huduma hiyo itamuwezesha mteja kutuma na kupokea fedha ndani na nje ya nchi pasipo makato yoyote.

Mkurugenzi Mkuu wa VISA Afrika Mashariki, Kevin Langley ametaja baadhi ya benki ambazo zimeshirikiana na VISA kutoa huduma hiyo kuwa ni pamoja na CRDB, NMB, NBC, Azania, TIB, Benki ya Posta, DCB, Benki ya Mkombozi, Mufindi Community Bank Limited, Benki ya Watu wa Zanzibar, Benki ya Uchumi, Benki ya Mwalimu, Benki ya Maendeleo na Yetu Microfinance Bank.

Akizungumzia uzinduzi huo, Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Dk. Bernad Kibese amesema ni hatua kubwa kwa taifa katika malipo ya kielektroniki na vilevile ushirikishwaji wa fedha.

“Uzinduzi wa Visa kwa njia ya simu ya mkononi unaonyesha hatua muhimu katika kuongeza kasi ya uhamaji kutoka fedha taslimu kwenda mfumo wa uchumi wa kidigitali Tanzania ambao ni mzuri kwa jamii zetu”. Ameeleza Naibu Gavana huyo.

Naye Rais wa Kampuni ya VISA Ukanda wa Kusini mwa Sahara, Aida Diara amesema lengo la uzinduzi huo ni kuboresha huduma na kupunguza makato yaliyopo kwa wateja, wafanyabiashara na sekta nzima ya fedha kwa ujumla.

“Matumizi ya malipo ya kieletroniki yanaongeza usalama na urahisi barani Afrika huku ikipunguza gharama na kuongeza uwazi katika shughuli za kifedha. Sehemu kubwa ya uchumi wa Afrika na usio rasmi, malipo hufanyika kwa kubadilishana fedha taslimu kwa zaidi ya asilimia 90. Inatia moyo kuona watanzania tayari wanafuata na kukubali teknolojia ya simu ikiwa na usajili wa watu zaidi ya milioni 41 na zaidi ya asilimia 80 ya waliosajiliwa hutumia mtandao kwa kutumia simu za mkononi. Ni ukweli unaofahamika kuwa zaidi ya watanzania milioni 20 wana usajili au akaunti za fedha kwenye simu. Hizi zote ni ishara za matumaini kwa VISA”. Amesema Diara.

 

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter