Madiwani kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Iringa mkoani humo wametoa pongezi kwa Halmashauri hiyo kwa kuendelea kuongoza kitaifa katika ukusanyaji wa mapato kwa kundi la Halmashauri za Manispaa hapa nchini. Diwani wa Mwangata, Edward Chengula amesema hatua hiyo inapaswa kupongezwa na kwamba ni ishara ya uwajibikaji mzuri wa watendaji wa Halmashauri hiyo chini ya Mkurugenzi wake Hamid Njovu.
Kwa upande wake, Naibu Meya wa Manispaa ya Iringa, Joseph Lyata amesema kuwa kuongoza kwa Manispaa hiyo katika makusanyo ya kodi ni ishara kuwa wananchi wameitikia wito wa serikali ya awamu ya tano wa kulipa kodi kwa maendeleo ya taifa .
Nao wabunge Ritta Kabati na Suzana Mgonakulima mbali na kupongeza manispaa hiyo kwa ukusanyaji wa mapato, pia wametoa pongezi kwa ujenzi wa vyumba vya madarasa ambavyo vimepelekea watoto wote kwenda shule na kupata elimu.
Mbali na kufanya vizuri katika ukusanyaji mapato, Manispaa ya Iringa pia ni moja kati ya Halmashauri ambazo zimefanya vizuri katika zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa na hivyo kuwezesha wanafunzi waliohitimu elimu ya msingi kuendelea na sekondari.