Home FEDHA Magufuli: Siwezi kununua halafu nyie mkate tena

Magufuli: Siwezi kununua halafu nyie mkate tena

0 comment 111 views

Rais wa Tanzania, John Pombe Magufuli amesema Halmashauri hazitakiwi kutoza ushuru kwa wakulima wa zao la korosho kwa sababu hazikuwasaidia kutafuta bei nzuri ya zao hilo. Rais Magufuli amesema hayo mkoani Mtwara wakati akizindua barabara ya Mtwara-Mnivata yenye urefu wa kilometa 50 na kueleza kuwa, serikali iliamua kununua korosho ili wakulima waweze kunufaika na kilimo chao, hivyo Halmashauri za mikoa ambayo inalima korosho zisitegemee ushuru kwenye zao hilo.

“Hakuna ushuru utakaokatwa kwenye korosho kwenda Halmashauri, kama mnategemea hilo, msahau, hamkufanya lolote kuwasaidia wakulima wakati wanahangaika na bei ya korosho hadi serikali tulipoingillia kati na kuamua kununua wenyewe, sasa siwezi kununua halafu nyie mkate tena pesa, sahauni”. Amesema Rais.

Pamoja na hayo, Rais Magufuli amesema wakurugenzi watakaopeleka maombi ya ushuru Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) watashughulikiwa kwa sababu ana mamlaka hayo. Kuhusu mradi wa barabara iliyozinduliwa, Rais Magufuli ameonekana kutofurahishwa na kazi ya mkandarasi na kuagiza asipewe kazi nyingine hadi amalize kujenga barabara hiyo.

“Namfahamu huyu Mkandarasi, mmepewa kazi mnasuasua na ninashangaa kwanini bado mnaendelea kuwapa wakandarasi wa ovyo kazi wakati mnajua wanasuasua, huyo tangu mwaka jana anahangaika na kilometa 50 hajamaliza hadi leo, sasa akipewa kilometa 200 si atajenga kwa miaka 200, sasa asipewe kazi nyingine hata kama ameshinda zabuni hadi amalize hii, sasa nyie wakandarasi wazalendo mmeingia kwenye kumi na nane zangu, ole wenu msifanye kazi”. Ameeleza kwa msisitizo Rais Magufuli.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter