Home FEDHA Mashirika yakumbushwa gawio

Mashirika yakumbushwa gawio

0 comment 130 views

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli amepokea gawio la Sh. bilioni 2.1 kutoka Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) jijini Dar es salaam. Akiwa makao makuu ya TTCL, Rais Magufuli ametoa wito kwa mashirika na taasisi za serikali 253 zilizopo kisheria kuhakikisha zinatoa gawio hadi kufikia Julai mwaka huu, ili kuepuka kuchukuliwa hatua za kisheria au kufutwa.

Rais Magufuli amemtaka Msajili wa Hazina, Dk. Athumani Mbuttuka kutuma barua kwa mashirika na taasisi hizo kuhusu agizo hilo, ikiwa ni pamoja na nakala itakayoenda kwa Katibu Kiongozi.

“Mashirika ambayo yanapaswa kutoa gawio nayaagiza ifikapo Julai mwaka huu yawe yameshatoa, vinginevyo tutatumia Sheria ikiwezekana kuyafuta, haiwezekani shirika kila mwaka liwe linapata hasara lakini halifungwi. Msajili wa Hazina yaandikie mashirika hayo yote na nakala iende kwa Katibu Kiongozi, haiwezekani taasisi kama jeshi la wananchi linatoa gawio halafu mengine yasitoe”. Ameeleza Rais Magufuli.

Pamoja na hayo, amebainisha kuwa fedha hizo zinatumika katika ujenzi wa shule, hospitali, miundombinu ya barabara pamoja na huduma nyingine za kijamii. Mbali na hilo, amefafanua kuwa kwa mwaka 2017/18 ni mashirika 40 yalitoa gawio lenye thamani ya bilioni 717.56 hivyo anategemea kwa mwaka 2018/19 idadi hiyo itaongezeka.

Vilevile, Rais amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa TTCL, Waziri Kindamba kuandika orodha ya mawaziri wanaotumia mtandao huo kwa sababu ni jambo la aibu kwa watumishi wa serikali kutotumia huduma za kiserikali na kutumia huduma za watu wengine.

“Mimi laini yangu ni TTCL, naomba naomba niletewe orodha ya viongozi wanaotumia laini ya TTCL, sio ziwapo tu bila kutumika, huwezi kulipwa mshahara wa serikali na hutumii mtandao huo, sijamaanisha msitumie mitandao mingine. Ofisi na Mashirika ya serikali natoa wito kwenu, muanze kutumia line za TTCL, lazima tuthamini vya kwetu”. Amesema Rais Magufuli.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter