Embu jiulize, ikiwa leo hii umekuwa milionea matumizi yako yatakuaje? Wengi wetu tunawachukulia mamilionea kama watu ambao wanaweza kupata kitu chochote kwa gharama yoyote ile kutokana na uwezo wao mkubwa kifedha. Inawezekana kuwa wana uwezo wa kupata vingi zaidi ya watu wa kawaida lakini sio kila kitu tunachosikia kuhusu watu matajiri ni cha ukweli.
Hapo chini ni vitu vitatu ambavyo kila mtu anatakiwa kufahamu kuhusu matajiri ya matumizi ya fedha zao. Tofauti na mawazo ya wengi, matajiri wengi kote duniani ni watu ambao wamefanikiwa kufika mahali walipo kutokana na kujifunza sehemu sahihi za kuwekeza na kuwa makini na matumizi yao.
Kwa watu wengi, ni kawaida kufikiria kuwa mamilionea ni watu ambao wanatumia pesa zao pasipo mpangilio maalum na bila kuwaza kuhusu kesho. Jamii inaamini kuwa kila milionea anakuwa na matumizi mabaya ya fedha kwa kuwa hana wasiwasi kutokana na kwenda ana kipato cha kutosha. Hii sio kweli. Inaelezwa kuwa matajiri wengi huwa na maisha ya kawaida na matumizi yao sio mabaya. Japokuwa wanaweza kumiliki vitu vya gharama, asilimia kubwa ya matumizi yao ya kila siku ni ya kawaida.
Kitu kingine ambacho jamii inatakiwa kufahamu ni kwamba, matajiri huwekeza sehemu ambazo wana uhakika kuwa zitawatengenezea fedha za kutosha baadae. Tofauti na wengi tunavyoamini, ukweli unabaki kuwa huhitaji kuweka fedha zako kila mahali ili kutengeneza zaidi. Hili ni jambo ambalo matajiri wengi huzingatia na hivyo badala ya kuwekeza kila siku na kuwa katika hatari ya kupata hasara, wanawekeza sehemu ambazo wanaziamini na wanajua zitawalipa. Mamilionea ni wawekezaji makini kuliko watu wanavyofikiria.
Jambo la mwisho ambalo unatakiwa kujua kuhusu watu wenye uwezo mkubwa kifedha ni, mamilionea wengi duniani walianza kama watu wa kawaida kutoka kwenye familia ambazo hazikuwa na utajiri. Ni kweli kuna wale ambao wamezaliwa katika familia zenye uwezo mkubwa kifedha na watakutumia fursa hiyo kutengeneza fedha zaidi lakini watu wengi wa kawaida hupanda juu kupitia jitihada zao na kutajirika. Sio kweli kuwa ‘unahitaji pesa kutengeneza pesa zaidi’. Wakati mwingine kinachohitajika ni bidii, mpango madhubuti, matumizi mazuri na elimu ili kuwa milionea. Kupitia kitabu chake cha I Can, I Must, I Will: The Spirit of Success marehemu Dk. Reginald Mengi ameeleza kwa kina jinsi familia yake ilivyokuwa maskini lakini licha ya changamoto zote alizokutana nazo, hakukata tamaa na alifanikiwa kuwa moja kati ya watu matajiri zaidi barani Afrika.
Licha ya kwamba mamilionea wengi wana uwezo mkubwa kifedha, wengi wao wameendelea kuishi maisha ya kawaida na kuwekeza fedha zao sehemu ambazo zina uhakika wa kuwalipa vizuri siku za mbele. Bila shaka wote tunaweza kujifunza kutokana na mambo hayo matatu. Kila mtu ana uwezo wa kuwa milionea ikiwa atazingatia vitu muhimu kama vile bidii katika kazi, uwekezaji wa uhakika na matumizi mazuri ya fedha kuanzia sasa.