Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) imeikopesha serikali Shilingi Bilioni 589.2 kwa ajili ya kutimiza mradi wa barabara ya lami yenye Kilomita 260 kutoka Kabingo hadi Manyovu mkoani Kigoma. Barabara hiyo inategemewa kumalizika mwaka 2025, ikiwa ni moja ya mikakati ya serikali ya awamu ya tano. Wakazi watakaokuwa wanaitumia bararaba hiyo watanufaika kimaendeleo kwa upande wa kiuchumi na kijamii pia kanda zitatengeneza uhusiano mzuri baina yao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, Doto James, amesema kuwa benki hiyo imekuwa ikishirikiana vyema na serikali ili kuhakikisha maendeleo ya nchi yanafanyika hususani katika upande wa miundombinu, hivyo wamechukua mkopo huo kutokana na unafuu wa masharti yake. Na endapo mradi huo utakamilika maendeleo ya kibiashara ndani nan je yataonekana.
“Mradi wa ujenzi wa barabara hii utakwenda sambamba na barabara ya Rumonge-Gitaza yenye urefu wa kilometa 45 nchini Burundi ili kuboresha mtandao wa barabara za Afrika Mashariki”. Amesema Katibu huyo.
Hata hivyo, ameongeza kuwa kukamilika kwa mradi huo kutaleta nafuu kwa wamiliki wa magari hasa katika kufanya matengenzo ya kila siku, na kuongeza usalama barabarani.
“Kama mnavyoelewa, miundombinu ya hizi barabara ni mibovu, hivyo gharama za matengenezo ya magari zinakuwa kubwa, tunapokwenda kuweka lami hizi barabara zitasaidia kupunguza gharama na hata ajali zitapungua” amesema James.