Home BIASHARAUWEKEZAJI Nini hasa huwavutia wawekezaji kuja Tanzania?

Nini hasa huwavutia wawekezaji kuja Tanzania?

0 comment 47 views

Uwekezaji ni moja kati ya sekta kubwa na nyeti nchini Tanzania. Hii inatokana na uhalisia kuwa ni moja kati ya sekta zinazoongoza kwa kuingizia taifa pato kubwa, kutokana na shughuli hii kujikita katika vipengele vingi vinavyogusa moja kwa moja uchumi wa taifa. Baadhi ya sekta ambazo zimekuwa zikiongoza kwa uwekezaji nchini Tanzania ni pamoja na sekta ya madini, kilimo, viwanda, utalii, uvuvi, elimu, teknolojia na ujenzi.

Kuna wawekezaji wa aina mbili, kwanza ni wawekezaji wa ndani kwa maana ya wazawa na wawekezaji wa nje yaani wageni. Kampuni mbalimbali kutoka nchi za nje zimefika nchini na kuanzisha miradi ikiwemo mashamba makubwa, viwanda, hoteli, shule na hata vyuo. Shughuli hizi kwa kiasi kikubwa zinasaidia katika kukuza uchumi wa taifa. Ni muhimu kutambua vitu vinavyowavutia wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini Tanzania badala ya kuwekeza katika nchi zao. Zipo sababu nyingi zinazopeleka wawekezaji wa nje kuja kuwekeza nchini. Kati ya sababu hizo ni pamoja na:

  1. Uwepo wa maliasili za kutosha. Muwekezaji yeyote anapenda kujihakikishia upatikanaji wa malighafi ya kutosha . Tanzania ina maliasili nyingi zinazowavutia wawekezaji. Sekta ya madini na utalii ni moja kati ya sekta kubwa nchini ambazo zimekuwa zikiongoza kwa kuwa na wawekezaji wengi wa nje. ( Ripoti ya Kituo cha Uwekezaji 2012)
  2. Sera na kanuni rafiki kwa wawekezaji. Serikali inapoweka sera nzuri na kanuni rafiki ni dhahiri wawekezaji wengi watakuja kuwekeza nchini. Sera na kanuni za uwekezaji zinamsaidia muwekezaji kujua malengo ya kuwekeza, jinsi uwekezaji utakavyoendeshwa na kusimamiwa, sambamba na kujua tahadhari za kuchukua wakati wa uwekezaji.
  3. Utulivu wa kisiasa. Hakuna mwekezaji wa kigeni anayeweza kuwekeza kwenye nchi yenye vita. Nchi nyingi zenye vita hazina wawekezaji wa kiuchumi. Utulivu wa kisiasa ni moja kati ya vitu vikubwa vinavyoshawishi wawekezaji wengi wa kigeni kuwekeza nchini. Historia nzuri iliyo nayo nchi ya Tanzania imeendelea kuifanya nchi yenye kupokea wawekezaji wengi wa kigeni kwa sababu ya utulivu na uwepo wa amani.
  4. Kigezo cha usafiri na miundombinu. Serikali imekuwa ikiboresha miundombinu na kuboresha huduma za usafirishaji ili kuendelea kuwavutia wawekezaji wa kigeni kuwekeza kwa wingi zaidi. Katika maeneo ya utalii na viwanda na migodini, serikali imekuwa ikijenga na kuboresha miundombinu ikiwemo barabara, viwanja vya ndege, reli na bandari. Mfano ni mwendelezo wa ununuzi wa ndege mpya ambao serikali ya awamu ya tano imekuwa ikifanya, sambamba na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).
  5. Soko la uhakika na upatikanaji wa nguvukazi. Uwepo wa soko hapa nchini ni moja kati ya vitu vinavyowavutia wawekezaji. Wawekezaji wengi wa kigeni wamewekeza katika sekta ya utalii kwa kujenga hoteli, na kampuni za misafara ya watalii kama ilivyo katika sekta ya madini kampuni nyingi zimeajiri wazawa kama nguvukazi na wengine wakiajiriwa kama wasimamizi na waratibu wa shughuli zote za migodini.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter