Mkurugenzi wa Benki ya CRDB Nyanda za Juu Kusini, Benson Mwakyusa amesema benki hiyo imeshatoa mikopo ya zaidi ya Sh. bilioni 60 kwa wakulima wadogo na wa kati ili kuunga mkono sera ya uchumi wa kati. Mwakyusa amesema wamekuwa wakitoa mikopo ili kuwainua wakulima pamoja na wananchi kiuchumi. Mkurugenzi huyo ameeleza kuwa baadhi ya wakulima waliofaidika na mikopo hiyo kuwa ni wakulima wa mpunga katika wilaya ya Mbarali na vilevile wakulima wa tumbaku wilaya ya Chunya.
“Lengo kubwa ya mikopo yetu kwa wakulima, wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo ni kuhakikisha wanainuka kiuchumi kama serikali ya awamu ya tano inavyotaka na kwa sababu tunakopesha zaidi vifaa dhamana yake muda mwingine huwa ni vifaa vyenyewe”. Amesema Mwakyusa.
Naye Meneja Mikopo wa CRDB kutoka makao makuu, Mussa Lwila ametaja sababu ya biashara nyigi kufa ni ukosefu wa elimu kwa wafanyabiashara ambao huiga biashara kwa watu wengine na kuchukua mikopo ambayo hushindwa kuilipa kutokana na biashara zao kutoendelea. Amewataka wafanyabiashara kuelimika ili kuepuka changamoto katika biashara wanazofanya.