Mikopo inakuja katika namna na ukubwa tofauti. Ikiwa mkopaji atakidhi vigezo na masharti ya sehemu anayoenda kukopa basi itakuwa rahisi kupata kiasi cha fedha anachohitaji.
Kabla hujakopa unatakiwa kujua kuwa kuna mikopo ya aina mbalimbali ikiwa ni pamoja na :
- Mikopo binafsi. Hii mkopaji hupewa mkopo hata kama ana historia mbaya ya kukopa au hajawahi kabisa kukopa.
- Mikopo ya biashara. Hii huwa ina masharti mbalimbali na vigezo hivyo ni muhimu kupata taarifa kamili katika taasisi husika ya kifedha unayoenda kukopa.
- Mikopo ya wanafunzi. Hii pia huwa na vigezo na masharti yake na hutolewa na serikali au watu/taasisi binafsi n.k.
Ni muhimu kuwa makini na suala la viwango vya riba. Jitahidi kujua viwango katika taasisi mbalimbali kabla hujafanya maamuzi ya kuchukua mkopo katika taasisi husika. Kuhusu muda unaotakiwa kulipa mkopo ni muhimu kujadiliana na taasisi husika kuhusu chaguo ambalo litakufaa au ambalo lipo ndani ya uwezo wako kwa sababu baadhi ya taasisi hutoza fedha zaidi ikiwa mkopaji atalipa mkopo mapema hivyo pata taarifa kuhusu mpango wa malipo na mabadiliko yakitokea.
Mbali na hayo, kabla ya kukopa unatakiwa kuangalia bajeti yako ilivyo, na unaweza kulipa mkopo kwa asilimia ngapi hii itakusaidia kuamua ni kiasi gani cha mkopo unaweza kumudu.
Kutokuwa na historia ya kukopa mara nyingi huwakosesha watu mikopo katika benki hasa wafanyabiashara. Bila kuwa na historia benki haiwezi kukupa fedha, hivyo kama una mpango wa kukopa kwa ajili ya biashara yako hususani katika benki hakikisha una historia ya kukopa na kurudisha.