Imeelezwa kuwa kiwango cha mikopo chechefu kimeshuka hadi asilimia 3.3, chini ya kiwango kinachovumilika cha asilimia 5.
Hayo yameelezwa na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba katika hafla ya futari iliyoandaliwa na BoT kwenye ofisi zake jijini Dar es Salaam Machi 20, 2025.

Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) Emmanuel Tutuba.
“Sekta ya fedha inaendelea kuwa na ukwasi wa kutosha, ambapo ukuaji wa mikopo kwa sekta binafsi ulifikia asilimia 16.8, ukizidi lengo la asilimia 15. Pia, kiwango cha mikopo chechefu kimeshuka hadi asilimia 3.3, chini ya kiwango kinachovumilika cha asilimia 5,” ameeleza Gavana.
Gavana Tutuba pia alieleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la huduma za kifedha katika miaka ya hivi karibuni, hali iliyochochewa na usimamizi mzuri wa sekta hiyo pamoja na kupitishwa kwa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018.
Hata hivyo, alikiri kuwa zipo changamoto chache zilizojitokeza katika sekta hiyo ya huduma ndogo za fedha, ikiwemo mikopo umiza, watoa huduma wasiokuwa na leseni (hasa wa mtandaoni), na shughuli za upatu.
Gavana Tutuba alibainisha kuwa ukuaji wa uchumi wa nchi ulifikia asilimia 5.4 kwa mwaka 2024, ukizidi wastani wa ukuaji wa uchumi wa dunia wa asilimia 3.2.
Ameeleza kuwa hali ya uchumi wa nchi inaendelea kuimarika, huku sekta ya fedha ikionyesha uimara na ukuaji thabiti.
“Tunaweza kujivunia kuwa uchumi wetu unaendelea kuimarika. Mfumuko wa bei ulibakia katika kiwango cha wastani cha asilimia 3.1, chini ya kiwango cha kimataifa cha asilimia 4.7, hali inayoashiria uthabiti wa sera za kifedha na uchumi wa nchi,” alisema Gavana Tutuba.
Alitoa wito kwa wananchi wote kujiepusha na shughuli za upatu na kuhakikisha kwamba wanapata huduma za fedha kutoka kwa watoa huduma wenye leseni ya Benki Kuu.
Kwa upande wake, Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuber Bin Ally, ameitaka Benki Kuu kuendelea kutoa elimu ya fedha kwa wananchi ili kuwasaidia kufanya maamuzi sahihi katika matumizi ya huduma za fedha.

Sheikh Mkuu na Mufti wa Tanzania, Dkt. Abubakar Zuber Bin Ally.
Ameeleza kuwa uelewa mzuri wa masuala ya kifedha utawasaidia wananchi kuepuka hasara zisizotarajiwa na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya fedha kwa manufaa yao na ya taifa kwa ujumla.
Vilevile, amewaasa wananchi kudumisha amani na utulivu, hususan katika mwaka huu wa uchaguzi, akisisitiza kuwa mshikamano na maelewano ni nguzo muhimu kwa maendeleo ya nchi.