Kampuni ya mikopo ya Kopafasta ambayo inalenga kuwakopesha wanachama waliosajiliwa katika mradi wa TACIP na PSG-P inayotekelezwa na Datavision International inayoshirikiana na taasisi na wizara za serikali imezinduliwa jijini Dar es salaam. Meneja wa kampuni hiyo, Patrick Kang’ombe amesema lengo la kampuni hiyo ni kuboresha sekta isiyo rasmi hususani zile za sanaa za ufundi na ulinzi ili kuwezesha walio kwenye sekta hiyo kupata mikopo ya fedha, vifaa na vitendea kazi, mafunzo ya usimamizi wa fedha, biashara na uwekezaji.
“Huduma yetu ni tofauti na pekee, tumechagua sekta zilizosahaulika zinazochukuliwa hazikopesheki, kwa kutokuwa na uwezo wa kuweka dhamana na kuaminika kwa mikopo”. Amesema Meneja huyo.
Pia ameongeza kuwa kampuni hiyo imeanzisha huduma hiyo ili kutekeleza sera na jitihada za serikali ya awamu ya tano kwa kupanua wigo wa walipa kodi, kuongeza pato la taifa, kukuza ajira, kuanzisha viwanda vidogo na kuwavuta wawekezaji. Kampuni hiyo imeshirikiana na wadau mbalimbali ili kuwezesha huduma hiyo, ambapo utumaji na ukopeshaji wa fedha unafanywa kwa njia ya simu ya mkononi ya Mlipa ili kumrahisishia mkopaji.