Home FEDHAMIKOPO Mikopo iwafikie wakulima

Mikopo iwafikie wakulima

0 comment 125 views

Mikopo inahitajika katika sekta mbalimbali za maendeleo zikiwemo biashara na kilimo. Mkulima huhitaji mkopo zaidi wakati anabadilisha mfumo wa ulimaji kutoka kwenye kilimo cha jadi/asili kwenda katika kilimo cha kisasa au cha biashara.

Karibu asilimia 70 ya watanzania wanajihusisha na kilimo. Wengi wao wanafanya kilimo kwa sababu imewabidi na hawana mtaji wa kuanzisha biashara nyingine. Hivyo ni muhimu kwanza kwa watu kubadilishwa mtazamo wa kuwa kilimo ni cha watu wasikini, pia kuelimishwa zaidi kuhusu kilimo cha kisasa ili kufanya kilimo chenye faida zaidi katika maeneo madogo.

Taasisi mbalimbali za fedha hapa nchini zikiwemo TADB, CRDB, FINCA na NMB zimekuwa zikiendelea kutoa elimu na kuwapa mikopo wakulima ili waweze kujiendeleza. Lakini wakulima wanatakiwa kuelewa kuwa wanahitaji mikopo kwasababu hizi:

Kubadili mfumo wa ulimaji. Mabadiliko haya huenda sambamba na mabadiliko ya matumizi ya fedha ikiwa ni pamoja na ununuzi wa mbegu, mbolea, dawa za kisasa na umwagiliaji. Hivyo ni ikiwa kwa namna moja au nyingine wanakwama basi hapo basi taasisi hizi zinapaswa kuwaunga mkono. Mkulima hatakiwi kuwa muoga kuchukua mkopo ili mradi tu awe ameweka malengo na mikakati madhubuti ili kuhakikisha analipa mkopo na kuendeleza zaidi kilimo chake na kuongeza mapato binafsi na ya nchi.

Vifaa ni muhimu. Taasisi za fedha zimeendelea kuwasaidia wakulima kupitia mikopo kupata miundombinu ya kisasa  ili kuendana na kasi ya teknolojia ikiwa ni pamoja na kuwakopesha wakulima matrekta kupitia vikundi, kujenga visima kwa ajili ya umwagiliaji nk. Taasisi za fedha zimeona kuna umuhimu wa kuwasaidia wakulima kupata vifaa stahiki ili kuwawezesha kupata mazao zaidi na hivyo kukuza uchumi wa taifa.

Kuwa na mikopo kutawasaidia wakulima kukabiliana na hatari zozote zinazoweza kutokea ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya bei, hali ya hewa nk. Kwa mfano wanaweza kukopa fedha kipindi cha kulima na kuzilipa kipindi cha mavuno au wanaweza kukopa kipindi ambacho wanazihitaji fedha hizo na kuzilipa wakati watakapouza mazao yao.

Sio kila mkulima anaweza kumiliki bima ya mazao. Serikali imepanga kuanzisha bima rafiki kwa wakulima wote hivi karibuni. Ikiwa wakulima bado watakuwa hawana uwezo wa kumiliki bima hizo au zinazotolewa na taasisi nyingine za bima basi wanaweza kukopa mkopo kwa ajili ya bima na kulipa mkopo huo pindi watakapopata faida.

Katika kuhakikisha mikopo inarudishwa, benki kama TADB zimejikita kuwatafutia wakulima masoko ili waweze kurudisha mikopo hiyo, ili iwasaidie wakulima wengine kitu ambacho ni kizuri kwani inakuwa rahisi kwao kupata masoko na kuacha kuuza kwa bei ya hasara.

Ili taasisi za fedha nchini ziwavutie wakulima wengi na watu wengine kukopa ni vyema kuweka masharti na riba rafiki katika mikopo wanayotoa. Watu wengi ni waoga wa mikopo na hukata tamaa mapema kwa sababu ya masharti magumu na riba kubwa. Elimu itolewe kwa makundi mbalimbali yanayojenga uchumi wa taifa ili mikopo zaidi iweze kutolewa na kuleta manufaa.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter