Home FEDHAMIKOPO Sababu za kukosa mkopo

Sababu za kukosa mkopo

0 comment 191 views

Katika maisha ya sasa kumiliki na kuendesha biashara inaweza kuwa ni jambo la kheri ikiwa mmiliki anapata faida na inaweza kuwa ni jambo la kuogopesha ikiwa mmiliki wa biashara hapati faida. Kuna mambo mbalimbali ambayo yanaweza kufanya biashara ifanikiwe au isifanikiwe.

Biashara nyingi hutegemea mikopo hasa katika kipindi kigumu. Na wakati mwingine wamiliki huandaa mazingira ya upanuzi wa biashara hata kabla ya kuomba mkopo hivyo ikitokea wameomba na kukataliwa, athari lazima zitokee katika biashara kwa ujumla.

Ni muhimu kujua kwanini maombi ya mkopo kwa ajili ya biashara yako yanaweza kukataliwa ili kuepuka kupoteza muda kwenye jambo lisilowezekana na badala yake kutafuta njia mbadala kupata fedha.

Baadhi ya sababu zinazoweza kupelekea maombi ya mkopo yakataliwe ni pamoja na:

Historia mbaya ya ukopaji

Mara nyingi watu hukataliwa maombi ya mkopo kutokana na sababu hii. Taasisi za kifedha hata watu binafsi huwa hawawezi kumuamini mtu ambaye ana historia ya kukopa bila kurudisha kwa sababu wanakuwa wanahatarisha fedha zao. Hata kama utakopeshwa licha ya kuwa na historia mbaya basi viwango vya riba lazima vitakuwa vikubwa sana. Kabla hujaomba mkopo wa biashara yako, jitahidi kuzingatia historia yako ya ukopaji. Kuwa na historia mbaya kutasababisha ukose mkopo na katika taasisi kama benki, kama huna historia kabisa ya kukopa unaweza kukosa mkopo pia hivyo hakikisha una desturi ya kukopa na kulipa ili kurahisisha ukopaji.

Biashara mpya

Kitu chochote kinavyoanza au kuanzishwa huhitaji muda kuzoeleka na watu. Baada ya kuzoeleka watu huanza kuamini uwepo wa kitu au jambo husika. Hivyo hali hiyo pia hutokea hata katika biashara na mikopo. Ikiwa biashara ndio kwanza inaanza lazima itakuwa vigumu kuaminiwa na taasisi za fedha kwa sababu ndiyo kwanza inaanza na hakuna historia inayoonyesha kuwa taasisi za fedha zinaweza kuiamini biashara hiyo na fedha zao. Kwa kuanza, unaweza kufanya malipo kwa mfano ya wachuuzi-mtoa huduma/bidhaa kupitia benki au taasisi nyingine za kifedha ili kutengeneza historia yako.

Hatari

Wakopeshaji huangalia pia aina ya biashara unayofanya kabla ya kukukopesha, ikiwa unafanya biashara yenye hatari kubwa hata kupata mkopo itakuwa shida kwani ni rahisi kwa biashara hiyo kushindwa. Kwa mfano biashara ya mgahawa ina hatari kubwa ya kushindwa hivyo hata ukipata mkopo masharti yatakuwa makali.

Kukosa dhamana

Kuna baadhi ya wakopeshaji huhitaji dhamana ili kutoa mkopo. Kwa kukosa dhamana stahiki unaweza kukosa mkopo kwa ajili ya biashara yako.

Mtiririko wa fedha

Jambo lingine linaloweza kupelekea maombi kukataliwa ni mtiririko wa fedha. Wakopeshaji hutaka kujua kama biashara yako inaingiza fedha za kutosha kulipa mkopo unaotaka kukopa. Kama mtiririko wako wa fedha hauridhishi basi uwezekano kupata mkopo huwa ni mdogo.

Kwa ujumla, katika ulimwengu huu wa digitali mambo mengi yamerahisishwa hivyo kuna taasisi mbalimbali ndani na nje ya nchi zenye vigezo na masharti kwa ajili ya wakopaji wa aina zote. Fanya utafiti ili kujua taasisi ipi inafaa kuomba mkopo kulingana na historia na mahitaji yako.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter