Mkuu wa Wilaya ya Rombo, Agnes Hokororo, amekabidhi mkopo wa Shilingi milioni 59 kwa vikundi 20 vya wanawake 479, mkopo huo usio na riba umetolewa na Halmashauri Wilaya ya Siha iliyopo mkoa wa Kilimanjaro.
Hokororo, ameeleza kuwa fedha hizo ni maelekezo ya serikali ambayo yanaeleza kila halmashauri kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani ili kuwasaidia vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kujikwamua kiuchumi.
“Akina mama niliowakabidhi mikopo leo tulianza kwa mafunzo ya ujasiliamali, ni vyema mkatumia mafunzo haya kujinufaisha kupitia fedha hizi na sio kwenda kuchangia harusi au kununulia vitenge” ameeleza Mkuu wa wilaya huyo.
Pia amewataka akinamama kuwa wabunifu wa biashara na kuacha tabia ya kuiga watu wengine ili kupitia biashara hizo waweze kujikwamua kiuchumi, vilevile amesisitiza wakinamama hao kuzirudisha fedha hizo kwa wakati ili ziweze kuwanufaisha wengine ambao hawajapata mkopo huo.
Aidha, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Siha, Valerian Juwal, ameeleza kuwa halmashauri hiyo imeshika nafasi ya sita kitaifa nay a pili kimkoa baada ya kutoa mkopo wa milioni 56 mwaka 2016/17. Mwaka 2017/18 imeshika nafasi ya tisa kitaifa na ya pili kimkoa ambapo wametoa sh milioni 45.
Naye, Ofisa Maendeleo wa Halmashauri hiyo, Alfoncina Makelele, amesema kuwa kutokana na mwamko mkubwa wa uundwaji wa vikundi, uhitaji wa mikopo ni mkubwa na fedha zilizopo ni ndogo. Pia ametaja changamoto nyingine ni baadhi ya vikundi vimekuwa vikichelewesha marejesho ya fedha hizo hivyo kukwamisha mgao wa mikopo hiyo kwa vikundi vingine.