Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF) Prof. Godius Kahyarara amesema shirika hilo limetenga zaidi ya Sh. 20 bilioni kwa mwaka wa fedha 2018/2019, fedha ambazo zimeelekezwa kwa ajili ya mikopo ya riba nafuu kwa wajasiriamali wadogo ili kusaidia kukuza uchumi wa viwanda.
Prof. Kahyarara amesema hayo wakati akizungumza na waandishi wa habari kwenye maonyesho ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Nyerere jijini Dar es salaam.
Mkurugenzi huyo ameongeza kuwa, NSSF imeingia makubaliano na benki ya Azania ili kuwezesha mikopo hiyo yenye riba nafuu ya asilimia 12.5 kwa lengo la kuwawezesha wafanyabiashara wadogo na kuongeza ajira kwa vijana.
Mikopo hiyo inatarajia kuwanufaisha wakulima, wavuvi, watu waliojiunga na vikundi rasmi vya uzalishaji mali kama vile Vicoba na SACCOS na AMCOS, pamoja na mamalishe na waendesha bodaboda.