Mtu yeyote anayetaka kuendelea kiuchumi anapaswa kuwa na tabia ya kuweka akiba na kutumia fedha kwa nidhamu na mpangilio. Suala la bajeti ni changamoto kwa watu wengi kwani wengi wetu hupenda kuweka mipango mingi kabla ya kupata fedha na pale zinapopatikana inakuwa ngumu kuweka bajeti na kujiwekea akiba.
Hivyo basi, inakupasa kwanza ufanye maamuzi ya kweli ili kuweza kuweka bajeti na kuachana na manung’uniko ya kila mwezi kwamba fedha hazitoshi.
Kwanza, unatakiwa kutambua fedha yoyote hata iwe ndogo kiasi gani ina thamani. Kwa hiyo, ni muhimu kuwa na utaratibu wa kuandika au kuweka rekodi ya mapato na matumizi yako ya fedha. Hii itakusaidia kuwa na nidhamu ya matumizi, hivyo kukupelekea kufanya bajeti na kujiwekea akiba.
Kila mtu ana malengo na ndoto za kufika sehemu fulani kimaisha na kiuchumi. Hivyo kupitia bajeti, mtu anaweza kutimiza ndoto hizo kwa kuandika malengo ya sasa na hata ya baadaye na kisha kufanya matumizi ambayo yanaendana na kipato chake. Ni muhimu kukumbuka kuwa bajeti haipo kwa ajili ya kukufanya ujinyime kila kitu, kwa maana hiyo, usijinyime sana, weka akiba kadri unavyoweza lakini hakikisha unamudu mahitaji yako ya kila siku.
Watu wengi hupuuzia bima, lakini kama una mpango wa kuandaa bajeti, inafaa kuwa na bima kwa mfano ya afya ili kupunguza gharama za ghafla na kuelekeza fedha ambazo ungetumia kwa wakati huo kwenye mambo mengine ya msingi.
Epuka matumizi yasiyokuwa na msingi. Hii huwa ni changamoto kwa watu wengi hasa vijana kwa sababu wengi wao wanashawishika kutumia fedha zaidi ya uwezo wao kwa vitu ambavyo si vya muhimu. Kama umeamua kujiwekea bajeti inafaa kuepukana na mambo hayo ili kuweza kujiwekea akiba zaidi.
Aidha, ili kufanikiwa katika uwekaji bajeti, ni vizuri kuepuka madeni kwa sababu unapoanza kuwa na madeni makubwa, inakupasa uelekeze fedha zako katika kuyalipa madeni hayo kuliko kuweka akiba ambayo itakusaidia siku za usoni.
Kwa ujumla, ili kuweza kuweka bajeti, inafaa ukitengeneza jedwali ambalo litakuwa linaainisha mapato, matumizi, akiba na unaweza kuongeza mengineyo. Hii itakusaidia sana kujua kama kipato chako kinaleta maendeleo au vinginevyo na nini cha kufanya ili kuweka mambo sawa.