Home FEDHA Pato halisi la taifa kufikia 7.3% mwakani

Pato halisi la taifa kufikia 7.3% mwakani

0 comment 78 views

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amesema serikali imeweka mikakati ya kuongeza kasi ya ukuaji wa pato la taifa na kufikia asilimia 7.3 mwaka 2019 ikiwa ni moja ya shabaha na malengo ya uchumi jumla. Waziri Mpango amesema hayo bungeni Dodoma wakati akiwasilisha Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Mpango na Bajeti ya Mwaka 2019/20

Katika maelezo yake, Dk. Mpango amesema kuwa katika robo ya kwanza ya mwaka 2018, pato halisi la taifa lilikua kwa asilimia 8.4 ambapo kati ya shughuli za kiuchumi zilizokua kwa kiwango kikubwa ni pamoja na ujenzi, habari na mawasiliano, usafirishaji na uhifadhi mizigo na kilimo.

“Serikali yetu imejipanga kuongeza kasi ya ukuaji wa pato halisi la taifa kufikia asilimia 7.3 kwa mwaka 2019 ikilinganishwa na matarajio ya asilimia 7.2 mwaka 2018 na kuongezeka kwa wastani wa asilimia 7.6 katika kipindi cha muda wa kati (2019/20 – 2021/22)” Amesema Dk. Mpango.

Aidha, Waziri huyo ameweka wazi shabaha na malengo mengine ya uchumi, yakiwemo ya kuendelea kudhibiti kasi ya mfumuko wa bei na kuhakikisha unakuwa kwenye wigo wa tarakimu moja ya wastani wa asilimia 5 katika kipindi cha muda wa kati pamoja na mapato ya kodi kufikia asilimia 12.7 ya pato la taifa mwaka 2019/20 na kupita matarajio ya asilimia 12.5 mwaka 2018/19.

Naye Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, George Simbachawene ameishauri serikali kuanzisha utaratibu wa kutenga kiwango cha asilimia moja ya pato la taifa maalum kwa ajili ya shughuli za utafiti na maendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter