Simba Sports Club na Serengeti Breweries Limited (SBL) wamesaini mkataba wa udhamini wa miaka mitatu wenye thamani ya Tsh bilioni 1.5 kupitia kinywaji chake cha Pilsner Lager.
Akizungumza wakati wa utiaji saini mkataba huo, Mtendaji Mkuu wa Simba SC Imani Kajula amesema “ni ubia wa nguvu kabisa, ubia wa Simba wawili. Hii ni package (kifurushi) ambayo imekuja wakati muafaka. Serengeti ni mbia mkubwa sana wa mpira wa Tanzania, huu ni mwendelezo wa kusaidia mpira.”
Amebainisha kuwa udhamini huo utasaidia uendeshaji wa klabu ambapo amebainisha kuwa gharama za uendeshaji wa vilabu huwa ni kubwa hivyo upatikanaji wa fedha ni muhimu sana.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa SBL, Obinna Anyalebechi amesema “tunajivunia kuziunganisha taasisi mbili kubwa za SBL na Simba kwa mkataba wa udhamini wa miaka mitatu. Kupitia udhamini huu utaifanya bia yetu ya Pilsner Lager kuwa mdhamini wa Simba.”
Amesema wanaamini kuwa udhamini huo utasaidia kukuza michezo nchini Tanzania.