Home FEDHA Serikali ya Tanzania yaweka mikakati uhaba fedha za kigeni

Serikali ya Tanzania yaweka mikakati uhaba fedha za kigeni

0 comment 141 views

Serikali imesema inaendelea kuweka mikakati na mbinu mbalimbali za muda mfupi, wa kati na mrefu katika kushughulikia changamoto ya uhaba wa Fedha za Kigeni (Forex).

Mikakati hiyo ni ikiwemo kuainisha baadhi ya sekta ambazo zinaweza kuleta mapato zaidi ambayo yatatoa suluhisho la kudumu la uhaba wa fedha za kigeni.

Waziri wa Fedha, Dkt. Mwigulu Nchemba ameeleza hayo wakati akifanya mazungumzo na Balozi mpya wa Uingereza nchini Tanzania, Marrianne Young aliyefika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha.

Dkt. Nchemba amesema kuwa katika bajeti inayoendelea, Serikali imeweka vipaumbele kwa baadhi ya sekta ambazo ni za kuongeza mapato ya fedha za kigeni japokuwa kama nchi kuna hali tofauti na baadhi ya nchi nyingine zinazoizunguka Tanzania kwakuwa inatekeleza miradi mikubwa ya kimkakati.

Ameongeza kuwa, hali hiyo imesababishwa na kutokuwa na uwiano katika uingizaji wa bidhaa nchini na uuzaji wa bidhaa nje ya nchi, lakini pia imetokana na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati kama mradi wa kuzalisha umeme wa Bwawa la Nyerere, mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) na Daraja la Busisi.

“Ni wazi kwamba kila unapokuwa na tofauti yoyote kati ya kile unachouza nje na kile unachoagiza kutoka nje, kutakuwa na shinikizo kwenye fedha za kigeni, na hicho ndicho kinachotokea na pia mikakati na hatua zinazochukuliwa zitasaidia kupata suluhisho la kudumu siku za karibuni,” amesema Dkt. Nchemba.

Aidha Dkt. Nchemba ametumia fursa hiyo kumpongeza Balozi huyo kwa kuteuliwa kuwa Balozi wa Uingereza nchini na kuahidi kuendelea kufanya kazi pamoja ili kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Uingereza katika kuhakikisha maendeleo endelevu ya kiuchumi.

“Dhamira ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuendelea kushirikiana na Serikali ya Uingereza ili kuimarisha ushirikiano muhimu wa maendeleo,” ameeleza Dkt. Nchemba.

Dkt. Nchemba amebainisha kuwa, Uingereza ni mdau muhimu wa maendeleo kwa kuendelea kutekeleza ajenda ya Maendeleo ya Kitaifa kama ilivyoainishwa chini ya Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 na Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano.

Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba akiwa na Balozi mpya wa Uingereza nchini Tanzania, Marrianne Young aliyefika Ofisini kwake Jijini Dodoma kwa ajili ya kujitambulisha.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter