Serikali imelipa jumla ya Shilingi trilioni 1.03 kati ya shilingi trilioni 1.41 za madeni ya wazabuni yaliyohakikiwa na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG) na kukidhi vigezo.
Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha, Hamas Chande ambapo amesema ni sawa na asilimia 73.
Chande ameeleza hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa Viti Maalum Ritha Kabati alietaka kufahamu Serikali imewalipa wazabuni wangapi wanaozidai Taasisi mbalimbali nchini na kiasi gani kimelipwa.
Chande amesema kuwa idadi ya Wazabuni waliolipwa ni 8,830 ambao walikuwa wakidai Taasisi mbalimbali za Serikali.
“Ulipaji huo ni hatua ya Serikali katika kuchochea uchumi na kukuza sekta binafsi,” amesema.
Amebainisha kuwa Serikali inaendelea kuwalipa wazabuni kwa kadri fedha zitakavyopatikana na pia ulipaji ni lazima ufuate taratibu kwa kuwa suala la zabuni hutolewa kwa mkataba na ni suala la kisheria.