Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Mifuko ya Jamii (SSRA) Dk. Irene Isaka amesema mamlaka hiyo inaendelea kupokea maoni kutoka kwa wadau mbalimbali pamoja na wananchi ambayo yatasaidia kuboresha kanuni na miongozo ya mstaafu kupitia mafao yake. Dk. Isaka amesema hayo jijini Dar es salaam na kufafua kuwa lengo la SSRA ni kuendelea na maboresho ya kanuni na miongozo na kuongeza kuwa dirisha la maoni lipo wazi kwa watanzania kuleta maoni yatakayosaidia kuboresha mfumo wa mafao kwa ajili ya wastaafu.
“Milango ipo wazi kwa wananchi na wadau mbalimbali kuleta maoni yao, ili tuboreshe sheria na kanuni zinazoongoza mifuko ya jamii na kuongeza tija katika mafao ya wastaafu”. Amesema Dk. Isaka.
Mkurugenzi huyo amesema tofauti na hali ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo pensheni za wastaafu zilikuwa na ukomo wa muda wa miaka 10 mpaka 12, kanuni za sasa zinamuwezesha mstaafu kupokea pensheni kwa kipindi chote cha maisha yake ya kustaafu na hivyo kumpa uhakika wa kupata mkopo na kuendelea kufanya miradi mbalimbali ya maendeleo.
“Moja ya majukumu ya SSRA ni kulinda na kutetea maslahi ya mwanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii hivyo tutaendelea kupokea maoni ili mwanachama anufaike zaidi kupitia michango yake atakapostaafu”. Amesema Mkurugenzi huyo.