Taasisi ndogo za fedha zimeundwa kwa lengo la kuwasaidia watu wa hali ya chini kupata fedha kwa ajili ya kujiinua kimaisha. Kutokana na kutokuwa na vigezo au kipato cha fedha cha kutosha kupata huduma za fedha ikiwa ni pamoja na mikopo, kuweka akiba katika taasisi kubwa kama benki ambazo huwa zina masharti na vigezo ambavyo mara nyingi watu wa hali ya chini hushindwa kuvimudu.
Inaelezwa kuwa zaidi ya bilioni 2 ya watu wazima na vijana takribani milioni 800 duniani kote hawana uwezo wa kupata huduma rasmi za kifedha. Idadi kubwa ya watu hawa imetoka katika nchi zinazoendelea ambapo aidha watu hawa hawana fedha za kutosha (wanatumia chini ya dola 2 kwa siku), benki haziko karibu na maeneo wanayoishi, hawana vigezo stahiki, hawana uwezo wa kukamilisha nyaraka kwa ajili ya kupata huduma katika taasisi rasmi za fedha, au hawajui faida zilizopo katika taasisi rasmi za kifedha.
Hadi sasa, watu wengi wamenufaika nchini kupitia na taasisi hizi ndogo. Kila mwaka taasisi kama FINCA, Tunakopesha Limited, African Microfinance Limited, Fanikiwa Microfinance, Brac na nyingine huandaa mafunzo, semina na mikutano mbalimbali kwa ajili ya wajasiriamali, wanawake, vijana na watu wanaoishi katika maeneo ya kijijini ili kuwapa elimu, ujuzi, mikopo, kuwajengea uwezo wa kuweka akiba kwa ajili ya maendeleo yao pamoja na ya jamii kwa ujumla.
Katika taasisi ndogo za fedha, wanaamini kuwa mtu akipewa kiasi kidogo cha fedha anaweza kubadilisha maisha yake na kuondokana na umaskini.
Taasisi nyingine huwa na viwango vikubwa vya riba, lakini kwa taasisi ndogo za fedha ni tofauti kidogo kwa kuwa viwango vipo chini ili kuwahamasisha watu wasio na uwezo kuchukua mikopo kwa lengo la kujiendeleza. Bado ni changamoto kwa wengi na ndio maana kuna mambo mengi ambayo yanatakiwa kurekebishwa ili kuleta urahisi kwa watu wote kunufaika. Hii ndio sababu watu wengi hushauriwa kuunda vikundi ili iwe rahisi kuweka akiba, kupata mikopo na vilevile kupewa elimu na mafunzo.
Taasisi hizi zimesaidia familia nyingi kwenye matumizi, ikiwa ni pamoja na masuala ya fedha za elimu. Kujihusisha na taasisi hizi maana yake ni mabadiliko ya kiuchumi hivyo hata kwa watu wanaoishi vijijini hupata urahisi wa kuwapeleka shuleni watoto kwa sababu wanakuwa wameshapata elimu, mafunzo na ujuzi wa kuweka akiba na kujiendeleza. Ni muhimu kwa taasisi hizi kuendelea kuwafikia watu wa hali ya chini ili kuchochea maendeleo hapa nchini.
Taasisi za fedha zinatakiwa kuendeleza nia yake kubwa ya kuendelea kuwafikia watu wasiokuwa na uwezo ili kupiga vita umaskini. Mwaka jana Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, alitangaza kuwa benki za CRDB, NMB, na Banc ABC zimekubali kupunguza viwango vya riba hivyo kuna matumaini kwa watu wanaotumia taasisi ndogo kupunguziwa pia viwango vya riba katika mikopo.