Home FEDHA Tanzania kusaini mkataba ukaguzi miamala ya kimataifa

Tanzania kusaini mkataba ukaguzi miamala ya kimataifa

0 comment 158 views

Serikali inatarajia kusaini mkataba ambao utaiwezesha Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kupata taarifa mbalimbali kutoka nchi 146 duniani ambazo zitasaidia katika kuongeza ufanisi wa ukaguzi wa miamala ya kimataifa.

Hayo yamebainishwa Bungeni jijini Dodoma na Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Hamad Hassan Chande, wakati akijibu swali la Mbunge wa Kisesa, Luhaga Mpina, aliyetaka kujua kiwango ambacho Serikali imejiimarisha kukagua miamala ya uhamishaji wa bei ya mauziano ya bidhaa na huduma baina ya kampuni za kimataifa.

Mkataba huo unajulikana kama (Multilateral Convention on Mutual Administrative Assistance in Tax Matters).

Chande amesema kuwa kwa kuzingatia vihatarishi vilivyopo kwenye miamala husika, Serikali imekua ikichukua hatua mbalimbali zinazolenga kuimarisha udhibiti na kuzuia upotevu wa mapato ikiwemo ya kuanzisha kitengo maalum cha usimamizi wa kodi za kimataifa.

“Mwaka 2011 Serikali ilianzisha kitengo maalum cha usimamizi wa kodi za kimataifa ndani ya TRA ili kuimarisha udhibiti na upotevu wa mapato,” ameeleza Chande.

Amesema hatua nyingine zilizochukuliwa ni pamoja na kuandaa na kusimamia utekelezaji wa kanuni na miongozo kuhusu ukaguzi wa kodi kwenye kampuni zenye uhusiano.

Pia Mamlaka ya Mapato Tanzania imenunua kanzidata ya Orbis kwa ajili ya kupata taarifa za kusaidia kufananisha bei za miamala ya kimataifa ili zisaidie katika ukaguzi wa kampuni zilizopo nchini.

Aidha amesema Tanzania imejiunga na jukwaa la kimataifa la ubadilishanaji taarifa za kikodi ili kuhakikisha kuwa inajenga uwezo wa kubadilishana taarifa za kikodi na nchi nyingine.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter