Ili kurahisisha miamala ya kifedha inayofanywa na wateja wao, Kampuni ya simu ya TTCL na Benki ya Watu wa Zanzibar (PBZ) zimeingia mkataba wa huduma ya T.Pesa. Mkuu wa Kitengo cha T.Pesa Tanzania, Alphonce Moses amesema huduma hiyo itawezesha wananchi kufanya miamala kwa ubora zaidi na kusema kuwa, huduma hiyo itatolewa masaa 24.
Mbali na kuwahakikishia wananchi kuwa huduma hiyo ni salama na rahisi, Moses pia amesema kuwa mfumo huo una faidi mbalimbali kwa watumiaji katika usalama wa fedha zao na vilevile hata kwa serikali katika kufahamu sekta za kutoa kipaumbele.
Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mtendaji wa PBZ, Khadija Shamte Mzee amesema benki hiyo inalenga kufikisha huduma katika maeneo yote na hadi sasa, tayari matawi mengi yameshafunguliwa Zanzibar na Tanzania Bara. Amewataka wananchi kuchangamkia huduma hiyo salama na kusema itawarahisishia wananchi kupata huduma na vilevile itaondoa kero ya kukaa kwenye foleni pale wanapohitaji kutoa fedha.
Mzee amesisitiza kuwa wananchi hawapaswi kuwa na wasiwasi na huduma hiyo kwani mkataba umepitiwa kwa umakini na hautakuwa na madhara yoyote kwao.