Kuwa milionea wakati wa kustaafu ni ndoto ya watu wengi. Lakini ni muhimu kujua kuwa ili kutimiza ndoto hiyo jitihada kubwa zinahitajika. Wakati mafanikio sio jambo la uhakika, hatua zifuatazo zinaweza kukusaidia kufikia malengo yako:
- Weka malengo
Hakuna mipango inayoshindikana kama mhusika atajipanga ipasavyo, jambo ambalo si kazi rahisi kwa wengi. Watu waliofanikiwa katika maisha walianza na mipango hadi kufikia walipofikia hivyo hakikisha una malengo na mpango mathubuti.
- Weka akiba
Bila akiba huwezi kufanikisha malengo yako. Watu wengi hushindwa kutimiza ndoto zao kwa sababu hawana akiba au mfumo wa fedha wa kufanya ndoto zao kwa vitendo. Sio rahisi kuweka akiba hasa kwa vijana kutokana na kukosa nidhamu ya fedha lakini ikiwa unataka kustaafu ukiwa na maisha mazuri basi anza kufanya hivyo mapema.
- Wekeza
Sio lazima uwe uwekezaji unaotoa faida za moja kwa moja, unaweza kuwekeza katika hisa au dhamana za muda mrefu ili uweze kunufaika mbeleni. Ni kweli kuna hatari ya uwekezaji wa namna hii lakini unatakiwa kujua kuwa hatari inapokuwa kubwa katika uwekezaji hasa wa hisa mafanikio yakipatikana nayo huwa ni makubwa. Hivyo utayari wako katika kukabiliana na hatari za uwekezaji utakusaidia kufurahia mafanikio baadae.
- Jiandae na dharura
Sehemu ya kuwa na mipango ya muda mrefu ni kujiandaa na dharura yoyote inayoweza kutokea. Kutokuwa tayari kubaliana na vikwazo vinavyoweza kutokea mbeleni kutasababisha ukate tamaa ya kuweka akiba kwa sababu itakubidi utatue kikwazo husika na fedha ulizoweka akiba. Kujiandaa mapema kutasaidia kutatua tatizo na kusonga mbele.
- Weka akiba zaidi
Kipato chako kinatakiwa kukua kadili muda unavyokwenda. Utapandishwa cheo, utahamia kampuni nyingine, utapata familia hivyo matumizi yatabadilika. Kila wakati unashauriwa kuweka akiba zaidi. Njia rahisi ya kufikia malengo ni kuwekeza kadri uwezavyo.
- Kuwa makini na matumizi yako
Likizo, gari, watoto na gharama mbalimbali ni matumizi makubwa. Ili kuongeza akiba yako jitahidi kupunguza matumizi. Hivyo ili kufikia malengo yako, jitahidi kuishi maisha ambayo yanaendeshwa na bajeti ili kuweka akiba zaidi.
- Mali na mikopo
Ni muhimu mara moja moja kujua hali ya mali ulizo nazo na mikopo unayodaiwa ili kujua namna utakavyoweza kuendesha mchakato mzima wa kifedha na kuhakikisha maendeleo yanafanyika na mikopo inalipwa ili kujijengea historia nzuri ya ukopaji.
- Fursa
Ni muhimu kutumia kila fursa inayokuja mbele yako. Kwa mfano kama kuna mashirika yanaruhusu watu kuweka akiba kwa ajili ya matumizi ya baadae basi jiunge ili kuweka akiba zaidi.
- Uvumilivu
Kuwa mvumilivu, mambo mazuri hayataki haraka. Kutenga muda, akiba na kuwekeza mapema ni baadhi ya mambo ambayo yatakufanya ufikie malengo yako na kuishi maisha mazuri baada ya kustaafu. Kuwahi kwako kuchukua hatua ndio kutaleta mafanikio kwa ukaribu zaidi.
Jambo la msingi ni kwamba, watu wengi huona miaka ya kustaafu ipo mbali sana hivyo hawana haraka kufanya mapinduzi ya kifedha. Ikiwa hukuanza kuweka akiba mapema, basi maisha yako yote utakuwa ni mtu wa kulalamika. Mipango na nidhamu ni nguzo muhimu za kutimiza malengo yako muda wa kustaafu utakapofika.