Mbunge Godbless Lema wa Arusha Mjini (Chadema) amesema kitendo cha kufungwa kwa maduka ya kubadilishia fedha (maarufu kama Bureau de Change) kutapunguza idadi ya watalii kufuatia usumbufu wanaokumbana nao kutokana na uamuzi huo. Lema amesema hayo bungeni Dodoma wakati akichangia taarifa za Kamati za Bunge za Miundombinu na Viwanda, Biashara na Mazingira.
Lema ameeleza Bunge, kuwa hakuna duka la fedha linabadilisha fedha jijini Arusha hivi sasa, hali ambayo inawalazimu watalii kusafiri hadi Moshi kupata huduma hiyo au kuingia benki na kubadili fedha zao. Ameongeza kuwa kutokana na adha hiyo, kampuni za utalii zinaamua kuwahamishia watalii nchi jirani ya Kenya ili kuepuka usumbufu. Mbunge huyo amesisitiza kuwa idadi ya watalii itapungua sana mwaka huu na kuhoji inachukuaje miezi miwili kurudishwa.
Mwishoni mwa mwaka jana, Benki kuu ya Tanzania (BoT) ilifungia maduka ya kubadili fedha jijini Arusha kwa makosa ya kuendesha shughuli zake bila kufuata utaratibu wa Sheria zinazosimamia biashara hiyo. Akiwa kikao cha kazi kati ya Rais John Magufuli, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) pamoja na wakuu wa mikoa, Gavana wa Benki Kuu Prof. Florens Luoga alisisitiza kuwa benki hiyo itaendelea kudhibiti biashara ya ubadilishaji fedha ili kuhakikisha sekta ya fedha haiyumbi.