Bunge la Tanzania limeidhinisha Bajeti Kuu ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha 2023/24 yenye jumla ya shilingi trilioni 44.39 ambapo mapato ya ndani yanatarajiwa kuwa shilingi trilioni 31.38, sawa na 70.7% ya bajeti yote.
Mapato yatakayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania yanakadiriwa kuwa shilingi trilioni 26.73 na mapato yasiyo ya kodi (Wizara, Idara, Taasisi na Mamlaka za Serikali za Mitaa) yanakadiriwa yatakuwa shilingi trilioni 4.66.
Akitangaza kura zilizopigwa, Spika wa Bunge la Tanzania, Dkt. Tulia Ackson Mwansasu, amesema kuwa wabunge 374 walikuwepo bungeni na wengine 18 hawakuwepo ambapo Bunge la Tanzania lina wabunge 393, akiwemo Spika.
Amebainisha kuwa wabunge 354 walipiga kura ya ndiyo, wabunge 20 walikuwa vuguvugu na hakuna mbunge aliyepinga Bajeti Kuu, ambapo matokeo hayo ni sawa na asilimia 95 ya wabunge wote walioikubali na kuipitisha.