Wafanyakazi wa kampuni ya East Coast Oils and Fats Limited jijini Dar es salaam wafanya mgomo wakidai kulipwa fedha kidogo, kucheleshewa mishahara yao na vilevile kunyanyaswa na uongozi wa kampuni hiyo. Akizungumza kwa niaba ya wafanyakazi wenzake, Ashura Mussa amesema kuwa kampuni hiyo imekuwa ikiwalipa pesa kidogo kupitia benki na kutokana na makato kuwa makubwa, pesa hizo zimekuwa hazikidhi mahitaji yao.
“Hatutaki kulipwa fedha hizo kupitia benki kwa sababu fedha yenyewe tunalipwa kidogo haiwezi kukidhi mahitaji yetu hivyo tunataka fedha zetu hizo zilizopotea turejeshewe”. Amesema.
Hata hivyo, wafanyakazi hao wameitaka kampuni hiyo kumuondoa msimamizi wao, Herry Simila kwa sababu amekuwa akiwatolea lugha za kashfa pale wakienda kuelezea changamoto zao. Simila hata hivyo, amekana shutuma hizo.
Mkurugenzi wa operesheni wa kampuni ya Upami Group Limited inayohusika na malipo ya wafanyakazi hao, Issa Lupangile amesema hadi kufikia tarehe 28 Februari, matatizo ya wafanyakazi hao yatakuwa yametatuliwa. Amewataka wafanyakazi hao kuendelea na kazi zao kama kawaida.