Wajumbe wa Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Uingereza (DFID) wamewatembelea baadhi ya wanufaika wa mpango wa Kunusuru Kaya Maskini wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) mtaa wa Dovya, Manispaa ya Temeke ambapo wanufaika hao wameeleza kuwa wanahitaji elimu ya kutunza fedha ili kufanya mipango endelevu. Katika ziara hiyo, wanufaika 21 walipatiwa fedha kupitia simu, 17 kupitia benki na 37 wamepokea moja kwa moja.
Ofisa Biashara wa TASAF Mwanahuba Meja ameeleza kuwa wanufaika hao wanajishughulisha na biashara kama iuzaji wa mahindi ya kuchemsha, ufugaji kuku, ushonaji na kuuza genge.
“Wapo waliopata changamoto mbalimbali za kuendesha biashara zao, lakini maofisa wamekuwa wakitoa mbinu mbalimbali lengo likiwa ni kuwasaidia kutumia fedha hizo kwa njia endelevu na kuwanufaisha”. Amesema Afisa huyo.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa kikundi cha Akiba na Mikopo cha TASAF Dovya Vicoba Group, Hadija Kilapo ametaja baadhi ya changamoto kuwa ni pamoja na baadhi ya wanakikundi kutohudhuria vikao.
“Wapo wanaofika katika vikao na kupewa mikopo lakini wanashindwa kuifanyia shughuli endelevu mwisho wanashindwa kurejesha kwa wakati, jambo linalozuia kujikomboa kiuchumi”. Amesema.
Naye, Mkuu wa ujumbe wa DFID, Eluka Kibona ametoa pongezi kwa TASAF kwa shughuli wanazozifanya hususani utoaji fedha kielektroniki kwa njia ya simu na benki.