Nchi ya Brazil imewekeza teknolojia pamoja na Dola za Marekani Milioni 9, sawa na Sh. Bilioni 21 za kitanzania katika mradi wa ‘Pamba Victoria’ ili kukuza soko la pamba katika nchi za Afrika Mashariki ambapo kwa sasa, wameanza na Tanzania, Kenya na Burundi.
Wakati wa mkutano wa kutathmini changamoto na mafanikio katika sekta ya pamba, Balozi wa Brazil nchini Tanzania, Antonio Cesar ameeleza kuwa mradi huo ulizinduliwa mwaka 2016 na kuanza rasmi 2017 kwa lengo la kukuza uzalishaji wa zao hilo.
“Tupo hapa kuitumia teknolojia inayotumika Brazil katika uzalishaji wa pamba, lakini sasa katika ardhi na mazingira ya Tanzania na Afrika Mashariki”. Amesema Balozi huyo.
Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Kilimo, Innocent Bashungwa ameeleza kuwa changamoto kubwa kwenye zao la pamba ni ufinyu wa viwanda vya kusindika japokuwa Tanzania ni moja kati ya nchi zenye uzalishaji mkubwa wa pamba barani Afrika. Bashungwa amesema kwa Tanzania, mikoa 17 na wilaya 56 hulima zao hilo lakini kutokana na kutotumia mbinu za kisasa, uzalishaji wake sio wa kuridhisha.
Kupitia mradi huo, Tanzania inategemea kuzalisha mara tatu zaidi ya inavyozalisha hivi sasa. Tanzania huzalisha kilo 300 kwa hekta moja huku Brazil ikizalisha kilo 4,200 kwa hekta.