Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imeanza kufanya usambazaji wa chanjo za UVIKO-19 katika mikoa yote Tanzania.
Ugawaji wa chanjo umezingatia taarifa ya visa vya wagonjwa waliohisiwa kuwa na UVIKO-19, idadi ya walengwa kwa kundi la kipaumbele pamoja na idadi ya chanjo zilizopatikana kwa sasa.
Katibu Mkuu Wizara ya Afya, Profesa Abel Makubi amesema hayo wakati akizindua ugawaji wa chanjo ya hiyo katika Bohari ya dawa MSD.
“Serikali kupitia mamlaka ya dawa na vifaa tiba (TMDA), Maabara ya Mkemia Mkuu, Maabara kuu ya Taifa, na vyombo vingine, vyote vimehakiki na kujiridhisha usalama na ubora wa hizi chanjo za Janssen kutoka kampuni ya Johnson & Johnson nchini Marekani,” amesema.
Amesema kutokana na mwongozo wa chanjo wa taifa dhidi ya Covid-19, Shirika la Afya Duniani (WHO), maelekezo ya COVAX FACILITY na upungufu wa uzalishaji wa chanjo toka viwandani, chanjo hizo kwa sasa zinatolewa kwa kufuata vipaumbele vya makundi yenye uhitaji mkubwa.
Ameyataja makundi hayo kuwa ni watumishi wa sekta ya afya, watu wazima umri wa miaka 50 na kuendelea na watu wenye magonjwa sugu.
“Kama ambavyo Serikali imekuwa ikieleza, uchanjaji kwa makundi yote nchini ni wa hiari au huru,” amesema.
Profesa Makubi amesema kwa kuwa chanjo zilizopokelewa kwa sasa hazitoshelezi walengwa wa makundi yote nchini, makundi mengine yatapata chanjo katika awamu inayofuata, mara zitakapowasili.
Chanjo hiyo inategemewa kuanza kutolewa kuanzia Agosti 3, 2021, katika vituo 550 vya kutolea huduma katika mikoa yote ambapo orodha ya vituo hivyo inapatikana pia katika tovuti ya wizara ya www.moh.go.tz.
Chanjo hizi zimeanza kusafirishwa jana mchana katika mikoa mbalimbali.