Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba Kabudi amesema nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) zimeingia makubaliano ya kuongeza uwekezaji wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kuwezesha upatikanaji wa matokeo ya afya kwa haraka na kutoa matibabu ya kibingwa.
Prof. Kabudi ameeleza hayo jijini Dar es salaam wakati akifunga mkutano wa nchi wanachama wa EAC uliokuwa ukijadili masuala ya afya na sayansi. Waziri huyo ameongeza kuwa katika kuta huduma hizo, mataifa ya EAC yanafikiria kuwa na vituo mahiri ambapo Tanzania itakijikita katika huduma za moyo na mishipa ya fahamu, Uganda katika saratani huku nchi ya Kenya ikijikitika kwenye figo.
Pamoja na hayo, mataifa ya Afrika Mashariki pia yamejipanga kupanua wigo wa upatikanaji dawa, kutumia huduma kwa mfumo wa digitali na chanjo. Aidha, Waziri huyo pia ametoa pongezi kwa jitihada zinazofanywa kuwainua vijana watafiti ili kuboresha mazingira ya utafiti kwa nchi wanachama.
“Kwa sasa ninawataka vijana wanasayansi watafiti wa afya katika Jumuiya ya EAC kuweka mkazo wa matumizi ya kidigitali, msome kwa kina kazi za wengine wenye ujuzi na sio kwa nchi husika pekee bali iwe ni kimataifa zaidi kwa kuwa yapo mengi na makubwa ya kujifunza”. Amesema Prof. Kabudi.