Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKI Mtanzania wa kwanza apata cheti eneo huru la biashara Afrika

Mtanzania wa kwanza apata cheti eneo huru la biashara Afrika

0 comment 112 views

Mfanyabiashara wa kwanza wa Kitanzania amepata cheti cha kufanya biashara katika eneo huru la biashara Afrika (African Continental Free Trade Area), AfCFTA.

Mfanyabiashara huyo Shabani Hamis ni kutoka katika kampuni ya kizawa ya EXPORT TRADING GROUP (ETG).

Kampuni hiyo imenufaika na mkataba wa soko hilo na kufanikiwa kusafirisha kontena 9 za kahawa ya Kitanzania aina ya Robusta ambazo ni sawa na tani 172.8 kwenda Algeria na kupata punguzo la kodi kupitia cheti cha uasilia wa bidhaa (Certificate of Origin) kinachotolewa na Chemba ya Wafanyabiashara wenye Viwanda na Kilimo (TCCIA).

Akikabidhi cheti hicho, Kaimu Mkurugenzi wa TCCIA Vicent Minja amesema cheti hicho kinamuwezesha mfanyabiashara huyo kupata punguzo la ushuru wa forodha kutoka asilimia 35 hadi asilimia 12.

“Tumekuwa tukiwaelimisha wafanyabiashara kuhusu faida za kuuza bidhaa nje kwa kutumia cheti hiki chini ya ACFTA na tumemkabidhi mfanyabiashara wa kwanza,” amesema Minja.

Mfanyabiashara huyo amepongeza juhudi kubwa zilizofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan za kuhamasisha uwekezaji na kuimarisha mazingira ya wafanyabiashara nchini ambazo zimeleta matokeo chanya katika ukuzaji wa biashara.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Ukuzaji Biashara kutoka Mamlaka ya Biashara Tanzania (TanTrade) Fortunatus Mhambe ametoa wito kwa Watanzania wengi zaidi kuendelea kujitokeza na kuchangamkia fursa zinazopatikana katika mpango wa eneo la Soko Huru Afrika.
Mhambe amewahamasisha Watanzania kuchangamkia fursa hizo za unafuu wa kodi zinazopatikana katika soko hilo, kwani hii itawasaidia Watanzania kutokuwa wasindikizaji bali watendaji na walaji wa fursa hizo, na kuwasihi Watanzania wengi zaidi wajitokeze TCCIA kuchukua Cheti cha Uhasilia wa bidhaa.

Ameeleza kuwa mbali na unafuu wa kodi, cheti hicho pia kitawasaidia kuongeza mitaji na kupanua uchumi wa mtu binafsi na Taifa kwa ujumla.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter