Rais wa Uganda, Yoweri Museveni amezitaka benki za biashara nchini humo kupunguza riba kubwa wanayotozwa wafanyabiashara. Rais Museveni amesema kuwa iwapo benki hizo hazitapunguza riba hadi asilimia 12, yeye binafsi atawahamasisha wafanyabiashara nchini humo kuacha kukopa kwenye taasisi hizo za kifedha.
Rais huyo, ameeleza kuwa wananchi wanapokopa, lengo huwa ni kuendeleza shughuli ambazo wanajipatia kipato ili waweze kujikwamua kimaisha lakini benki nchini humo zimekuwa zikiwanyonya wafanyabiashara wadogo na wajasiriamali badala ya kuwasaidia, hali ambayo haipaswi kufumbiwa macho.
Aidha, Rais Museveni amesema ana mpango wa kuongeza fedha katika benki ya biashara ya Uganda ili pale wafanyabiashara na wajasiriamali watakapohama kutoka benki hizo, wahamie katika benki ambayo wanaweza kuomba mikopo kwa riba ndogo isiyozidi asilimia 12.
“Zinakopesha kwa riba kati ya asilimia 20 na 24, huu ni wizi mkubwa. Ni wakati sasa kuziaga benki za aina hii. Mnakopesha fedha nyingi kwa wafanyabiiashara wakubwa wanaokwenda China badala ya kuwainua wajasiriamali ambao ndio wengi zaidi”. Ameeleza Rais Museveni.