Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema taifa la Tanzania linaongoza kwa uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja katika ukanda wa nchi za jumuiya ya Afrika ya Mashariki (EAC). Majaliwa amesema hayo katika kongamano la biashara kati ya Tanzania na China na kuongeza kuwa Tanzania imejipanga kufanikisha azma ya uchumi wa viwanda.
“Mtiririko wa uwekezaji wa kigeni wa moja kwa moja nchini umeongezeka kwa zaidi ya miaka 10 iliyopita na sasa wawekezaji wameipa kipaumbele Tanzania kama kitovu cha uwekezaji barani Afrika”. Ameeleza Majaliwa jijini Beijing, China.
Kwa mujibu wa ripoti ya uwekezaji duniani iliyotolewa mwaka 2018, Tanzania imepokea takribani Dola bilioni 1.2 za Marekani mwaka 2017 na inaongoza kwa kupokea uwekezaji katika ukanda wa Afrika Mashariki. Katika maelezo yake, Majaliwa amesisitiza kuwa Tanzania inafanya jitihada kubwa kufikia uchumi wa kati ifikapo 2025, hivyo imeweka mkazo mkubwa katika kujenga msingi imara wa viwanda.
Mbali na hayo, Waziri Mkuu pia amezungumzia sekta ya fedha kwa ujumla na kusema Tanzania inawakaribisha wawekezaji kuanzisha taasisi za kifedha kwa ajili ya kutoa mikopo midogo, benki za uwekezaji, benki za kilimo pamoja na benki za biashara. Aidha, Waziri Majaliwa amesisitiza uwepo wa fursa lukuki kwenye sekta ya huduma hususani katika teknolojia ya habari na mawasiliano (Tehama) ambayo ni moja kati ya sekta ndogo zinazokuwa kwa kasi hapa nchini.