Kila nchi duniani ina malengo ya kutengeneza magari yake na kupunguza kuagiza nje ya nchi, lengo hilo limetimia Uganda ambapo wameanza kufanya majaribio ya gari iitwayo Kiira EVS. Kupitia kampuni ya Kiira Motors Corporation (KMC) wamekamilisha kutengeneza gari hiyo ambayo inatumia mafuta na kampuni hiyo inategemea kufanya majaribio umbali wa kilomita 1,600. ambapo operesheni ya majaribio ikikamilika italeta fursa ya biashara kati ya Uganda na nchi nyingine.
Meneja wa Maendeleo ya Biashara (KMC) Allan Muhumuza amesema majaribio hayo yameanza jiji la Kampala, na kuendelea katika miji ya Masaka, Mbarara, Kabale, na Kisoro huku wakiwa na mpango wa kuendesha gari hilo hadi magharibi ya Uganda.
“Tumeandika historia. kote tulikopita, kuanzia Kampala, watu hawaamini kama ni gari lililotengenezwa katika ardhi ya Uganda tunategemea kuendelea na majaribio kwa kilomita 1,600 zaidi”. Amesema Meneja huyo.
Hadi sasa Uganda ina magari mengine kama Kiira EVE ambalo linatumia umeme tu, na lingine ni basi ambalo linatumia umeme jua linaitwa Kayoola. Pia wana mpango wa kutengeneza magari mengi zaidi kwenye kiwanda chao kilichojengwa kilomita 100 katika mji wa Jinja ili kuteka soko la Afrika Mashariki na nchi nyingine zitakazotaka kufanya biashara ya magari na nchi hiyo. Aidha mradi huo unategemea kuwanufaisha wananchi 2,000 kupitia ajira za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja ajira 12,000.