Biashara hizi zinalipa

0 comment 185 views

Sio kila biashara inahitaji mtaji mkubwa. Kuna biashara ndogo ambazo zimewatoa watu wengi kimaisha kutokana na jitihada zao pamoja na kufanya kazi kwa bidii.

Ikiwa huna sehemu ya kujiingizia kipato ni muhimu kutafakari namna ambayo inaweza kukuingizia fedha na mara nyingi unashauriwa kufanya jambo unalolipenda ili upate hamasa ya kufanya shughuli hiyo. Kwa jiji la Dar es salaam, kuanzisha biashara ni rahisi kwa sababu kuna soko kubwa hivyo unaweza kuuza bidhaa au huduma sehemu yoyote ili mradi iwe inavutia wateja.

Zifuatazo ni biashara nne ambazo unaweza kuanzisha kwa mtaji mdogo tu:

Juisi na Matunda

Biashara hii imewatoa watu wengi sana na mahitaji ya wateja hayapungui kwa sababu wananchi wengi wamekuwa wakitumia vyakula visivyokuwa salama kwa afya zao, hivyo kila wakimuona mtu anauza matunda au juice moja kwa moja hupata hamu ya kumuungisha muuzaji. Ili kujipatia wateja wengi kwanza unatakiwa kuhakikisha maandalizi ya juisi au matunda yako ni nadhifu na yanamhamasisha mnunuaji kununua. Unaweza kuuza juisi na matunda yako aidha kwa kutembeza katika maeneo ya kazi za watu au unaweza kuuza kupitia mitandao ya kijamii. Jambo la muhimu ni usafi na ukarimu kwa wateja kwa sababu ukiwa mkarimu basi wateja wataendelea kuja. Baadhi ya watu walionufaika na biashara hii ni mfanyabiashara ‘Mak Juice’ ambaye alianza na mtaji wa Sh. 7,000 tu.

Supu

Ikiwa una fedha kidogo unaweza kutumia fedha hizo kununua mahitaji na kuandaa supu ambayo una uhakika unaweza kuiandaa nyumbani, baada ya hapo kwa sababu unaanza unaweza kupitisha katika maeneo ya kazi za watu. Kama ilivyo kwenye matunda na juisi hata katika biashara hii ni muhimu kuwa msafi na mkarimu ili uweze kujipatia wateja wengi zaidi. Watu wengi walianza kidogo na wamefanikiwa kuanzisha sehemu zao maalum kwa ajili ya biashara hii. Ikiwa una smartphone, ni muhimu kutumia mitandao ya kijamii ipasavyo.

Nguo

Hii inawafaa hasa wanawake kwa sababu nguo zao zinapatikana kwa wingi na kwa bei rahisi. Hivyo ikiwa ni mpangiliaji mzuri wa nguo na unajua nguo ipi nzuri na ipi si nzuri, unaweza kuchangamkia fursa hii kwa kwenda maeneo ambayo nguo huuzwa kwa bei poa. Hapa pia mitandao ya kijamii ni muhimu. Vilevile, usipangilie bei kubwa hasa kwa nguo za mitumba. Lengo ni kupata wateja na itapendeza kama ukiwa mbunifu wakati wa kuzitangaza nguo zako. Kwa mfano badala ya kuuza nguo iliyokunjana, unaweza kunyoosha nguo zako ili zipate muonekano mzuri, pia unaweza kupiga picha katika mazingira mazuri ili kumhamasisha mteja.

Kahawa

Tumezoea kuona watu wanatembeza kahawa mitaani. Kwa upande mwingine biashara hii inaweza kuanzishwa kwa unadhifu zaidi na muanzishaji anaweza kujipatia mafanikio. Kama inavyojulikana,kwenye juisi kuna vikombe ambavyo mteja anaweza kuondoka navyo. Hivyo kwa mtaji usiozidi Sh. 100,000 inawezekana kufanya biashara hii ukiwa nyumbani. Ikiwa unataka kufanya biashara hii ni vyema ukiwa na wateja wa aina fulani ili iwe rahisi kufikisha huduma. Ubunifu pia ni muhimu kuna kwani kuna aina nyingi ya utengenezaji kahawa

Fursa ni nyingi sana. Jambo la muhimu ni kuwa mbunifu na mtu ambaye yuko tayari kufanya mabadiliko na kuanzisha vitu vipya. Huduma au biashara yako ikiwa inahamasisha wateja, bila shaka utapata soko kubwa.

Leave a Comment

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter