Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi na Ajira, Anthony Mavunde ametoa wito kwa vijana kuwa wabunifu na wathubutu katika kujiajiri kwa kuthamini kazi wanazofanya. Mavunde amesema hayo wakati wa ufunguzi wa wiki ya vijana kitaifa inayofanyika jijini Tanga katika viwanja vya tangamano na kuongeza kuwa, vijana wanatakiwa kuthamini shughuli wanazofanya na kuziwekea kipaumbele ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuondokana na dhana ya kuajiriwa.
“Vijana muondokane na mawazo mgando kutegemea kuajiriwa badala yake wajikite katika kujiajiri na serikali itawapa mikopo kwa ajili ya kukuza mitaji na kuboresha mazingira ya shughuli mnazofanya”. Amesema Mavunde.
Naibu Waziri huyo pia ametumia fursa hiyo kuwasisitiza vijana kujitokeza kwa wingi katika sherehe za kilele cha mbio za mwenge zitakazofanyika Oktoba 14, katika viwanja vya Mkwakwani, mjini humo.