Na Mwandishi Wetu
Mkuu wa Wilaya ya Mtwara Evod Mmanda amewataka vijana wilayani humo kuchangamkia fursa ya urasimishaji ujuzi inayotolewa na Mradi wa Uwezeshaji Vijana Kiuchumi (YEE) kwa kufanya kazi kwa ushirikiano ili waweze kuondokana na tatizo la ajira nchini. Mmanda amesema mradi huo umekuwa ukiwapa ujuzi vijana kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kuwaongezea uwezo katika stadi mbalimbali ili waweze kujiajiri.
Mradi huu umepanga kugusa zaidi vijana wanaotoka katika familia zisizojiweza na wenye kipato kidogo hasa wasichana na walemavu ili kuwapatia nafasi ya kuboresha maisha yao na kuwawezesha kutumia ujuzi wao na kuleta tija ndani ya jamii.
Mratibu wa Mafunzo wa mradi huo Nurdin Amri amesema mpaka sasa vijana 1,500 wameshafikiwa katika Wilaya ya Mtwara. Mradi huu umelenga kuwezesha vijana kati ya miaka 15 hadi 35 ili kuwaepusha na mazingira hatarishi.