Meneja wa Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (SIDO) jijini Arusha, Nina Nchimbi ametoa wito kwa wajasiriamali kuboresha vifungashio vinavyotumika kwenye bidhaa zao ili kupanua wigo wa biashara zao. Meneja huyo amesema hayo wakati wa kufunga mafunzo ya siku saba ya utengenezaji sabuni, dawa za kuua wadudu pamoja na zile za kusafisha vigae na kueleza kuwa wajasiriamali wanatakiwa kuwa wabunifu wakati wa uzalishaji ili kuongeza ubora ambao utawavutia wateja kutoka ndani na nje ya nchi.
“Unapozalisha bidhaa yako kila wakati inakuwa na muonekano ule ule, inakuwa ngumu kupata wateja wapya, hivyo ili muweze kupata wateja wapya ni lazima mbadili muonekano wa vifungashio hivyo view vya tofauti na viweze kuvutia wateja na kwa kufanya hivyo, mtapata soko la uhakika”. Amesema Nchimbi.
Kwa upande wake, Mkufunzi wa mafunzo hayo Bahati Mkopi amesema amesema takribani wajasiriamali 80 wamehitimu mafunzo hayo na kufanikiwa kuanzisha viwanda vidogo zaidi ya kumi. Mkopi amedai mafunzo hayo yamewezesha wananchi hasa vijana kujiajiri. Baadhi ya wajasiriamali waliopata mafunzo hayo wametaja baadhi ya changamoto wanazokumbana nazo kuwa ni pamoja na uhaba wa malighafi na upatikanaji wa vifungashio. Wameshauri wadau mbalimbali na vilevile serikali kupitia SIDO kuboresha mazingira ya wawekezaji ili waweze kupata mahitaji hayo kwa urahisi zaidi.