Home HABARI ZA AFRIKA MASHARIKIUJASIRIAMALI UMEJIPANGA VIPI BAADA YA KUSTAAFU

UMEJIPANGA VIPI BAADA YA KUSTAAFU

0 comment 135 views

Inawezekana bado hujafikia umri wa kustaafu kazi lakini bila shaka umeshuhudia jinsi watu wengi ambao wamestaafu wakipata tabu na kulalamikia ugumu wa maisha. Asilimia kubwa ya wastaafu hapa chini wanaishi maisha ambayo kiukweli hayaridhishi kwani wengi wamekuwa wakitegemea pensheni yao kuendesha maisha. Kama vijana, lazima tuweke akilini kuwa miaka inaenda na siku za kuajiriwa zitafika kikomo. Hiyo ndio hali halisi ya maisha. Lakini je, tumejiandaa na maisha kama wastaafu?

Kama muajiriwa hivi sasa umejipangaje kukabiliana na maisha, familia na majukumu pindi ukistaafu? Utategemea pensheni pekee? Fedha hiyo itakidhi mahitaji yako yote? Wengi waliopo katika soko la ajira hivi sasa huwa wanafanya kosa moja kubwa ambalo huwatokea puani baadae. Hawaweki akiba kuanzia mwanzo. Wanatumia fedha bila kuwa na mipango ya baadae hivyo pindi wanapotoka katika soko la ajira wanaishia kutegemea kiasi kidogo cha fedha wanachokipata kama pensheni.

Ili kuepuka na changamoto za kifedha baadae, ni vizuri kama ukijifunza kuwekeza katika miradi ambayo itakuingizia fedha hata baada ya kumaliza muda wako katika ajira unayofanya. Unaweza kuwekeza katika kilimo, ujasiriamali, biashara ndogondogo au chochote kile kitakachoingiza fedha kulingana na mazingira uliopo. Kabla ya kufikia umri wa kustaafu ni muhimu kuwa na elimu ya kutumia fedha kimaendeleo, uwekezaji na ujasiriamali ili hata baada ya kazi uwe na chanzo kingine cha kuingiza kipato mbali na pensheni.

Vilevile, ili kuokoa fedha nyingi ni muhimu kuwa na bima ambayo itasaidia kupunguza gharama. Katika kuhakikisha wewe na familia yako mtakuwa na maisha mazuri hata baada ya kustaafu ni lazima kujiunga na bima ili hata majanga kama magonjwa, moto au ajali yakitokea, unakuwa na uhakika wa kupata huduma kwa haraka na urahisi pasipo kuwa na mawazo ya fedha au pensheni. Katika mazingira kama haya kuwa na bima ni muhimu sana kwani badala ya kutumia fedha nyingi katika matibabu kwa mfano, unaweza kutumia fedha hizo katika mambo mengine ya maendeleo.

ADVERTISEMENT

Jamii kwa ujumla inapaswa kujifunza kutokana na makosa ya wastaafu waliopita. Tuweke mazingira bora kwa ajili ya maisha ya baadae. Waliopo katika soko la ajira wafahamu kuwa kuna maisha baada ya ajira. Tuepuke na matumizi mabaya ya fedha na tujifunze kuweka akiba kuanzia mwanzo. Elimu kuhusu njia sahihi za kutumia mafao itolewe kwa wastaafu ili kuwaweka katika nafasi nzuri zaidi kiuchumi.

Serikali nayo haipaswi kufumbia macho changamoto wanazokumbana nazo wastaafu wanapofuatilia mafao yao. Kuwepo na utaratibu maalum kwa wastaafu ili wapate haki zao bila usumbufu wowote. Kama tulivyowathamini wakati walipokuwa wakijenga taifa, tuendelee kuona mchango wao katika taifa hata baada ya muda wao katika ajira kumalizika.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter