Na Mwandishi wetu
Mfuko wa Rais wa Kujitegemea (PTF), wakishirikiana na Kanisa la Kiinjili la Kilutheri(KKKT), Ushirika wa Kigogo wamewapatia mafunzo na mikopo vijana walioachana na matumizi ya dawa za kulevya.
Vijana hao wapatao 20 ambao walikuwa chini ya uangalizi wa Mchungaji Richard Hananga, wamepatiwa msaada huo kama jitihada mojawapo ya wao kuendeleza mawazo ya kibiashara waliokuwa nayo na kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa,
Mkurugenzi Mkuu wa mfuko huo, Haigath Kitala amewaambia waandishi wa habari jijini Dar es salaam kuwa ofisi yao imetoa mikopo yenye thamani ya Sh milioni nne kwa vijana hao walioachana kabisa na madawa ya kulevya. Pia kabla ya kuwapatia fedha hizo, walielimishwa juu ya namna za kufanya shughuli mbalimbali na kwamba wanaendelea kuwafuatilia vijana hao kwa karibu kwani kuna mpango wa kuwapeleka Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA) ili kuwaendeleza zaidi.
Mmoja wa vijana aliyefaidika na mkopo huu ametoa shukrani zake kwa Rais John Magufuli kwa kuwezesha mfuko huo kumsaidia kwani sasa anafanya biashara na kusaidia familia yake bila matatizo.