Serikali imewaalika waandaji wa Mkutano na Maonesho ya Kimataifa ya Kilimo na Chakula (International Agri Food Conference and Exhibition) kujadiliana namna ya kurasimisha shughuli hizo ili ziendane na maonesho ya Kimataifa ya Kilimo Nanenane yanayofanyika nchini kila mwaka.
Waziri wa Kilimo Hussein Bashe ameyasema hayo Agosti 2023, wakati wa ufunguzi rasmi wa maonesho hayo, jijini Dar es Salaam.
Bashe amesema amefarijika kuona washiriki na bidhaa zinazooneshwa kuendana na matukio ya Nane Nane nchini ikiwa ni pamoja na kukutana na wakulima, wachakataji na wafanyabiashara kutoka nchi mbalimbali za bara la Asia.
“Baada ya kujionea uwiano wa maonesho haya na ya kwetu ya Nane Nane, nimeona ni vema nikutane na waandaji kurasimisha ushirikiano wa pamoja na Serikali kwa kuyavuta maonesho haya nchini kuanzia mwaka kesho,” ameeleza Waziri Bashe.
Ameongeza kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho za kuingia katika makubaliano na Serikali ya India ili kuwa na ubia kwenye uzalishaji wa mazao, tafiti na mafunzo.