Waziri wa Kilimo, Japhet Hasunga ameagiza Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) kuhakikisha kuwa katika msimu wa kilimo 2019/2020, unanunua mahindi kwa zaidi ya tani 500,000 kutoka kwa wakulima ili kuiwezesha serikali kutimiza azma yake ya kuimarisha masoko yao.
Waziri Hasunga ameeleza hayo jijini Dodoma katika hafla ya kukabidhi mtambo wa kusafisha nafaka kwa NFRA kutoka kwa Mpango wa Chakula Duniani (WFP). Pamoja na hayo, pia ameitaka NFRA kubadilisha mfumo wake wa kununua mahindi ili kupunguza gharama kubwa zinazojitokeza.
Aidha, Hasunga amedai Wakala huo umekuwa ukinunua nafaka kiduchu kutoka kwa wakulima kwa ajili ya kuhifadhi pekee na kuwataka kufanya biashara ya kununua na kuuza nafaka kwa wingi.
Katika maelezo yake, Waziri huyo amesema kwa kipindi kirefu, WFP imekuwa mdau mkubwa wa maendeleo nchini na kumhakikishia Mwakilishi Mkazi wa WFP, Michael Dunford kuwa hawakukosea kuichagua Tanzania kuwa Kituo cha Usimamizi wa Bidhaa za Kimataifa (GCMF) kwani kupitia kituo hicho, wakulima wanapata masoko ya uhakika kwa ajili ya mazao ya chakula.