Wasambazaji wa pembejeo za kilimo pamoja na maofisa kilimo wameanza kupokea mafunzo kuhusu namna ya kutumia mbolea kwa njia sahihi ili kuwasaidia wakulima kuongeza tija katika kilimo wanachofanya. Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa kampuni ya Petrobena East Africa Sabena Kubini amesema wanatoa mafunzo hayo ili kuwajengea uwezo wasambazaji wa pembejeo na kuboresha uzalishaji.
Kubini amedai wanatoa mafunzo kwa wanaosambaza mbolea, wakulima na maofisa kilimo ili kuwapa uwezo wa kuongeza uzalishaji kwa kutumia mbolea zilizo na virutubisho linganifu ambapo mpaka sasa, takribani maofisa kilimo na wasambazaji 50 kutoka mkoani Morogoro wameanza kupatiwa mafunzo hayo.
Mkurugenzi huyo pia amesema kuwa tafiti mbalimbali zinaonyesha uzalishaji mdogo kutokana na wakulima kushindwa kufahamu aina sahihi ya mbolea pamoja na matumizi yake hivyo kupelekea udongo kukosa rutuba.