Home KILIMO MBINU ZA KUONGEZA UZALISHAJI

MBINU ZA KUONGEZA UZALISHAJI

0 comment 118 views

Katika kilimo uzalishaji ukiwa wa uhakika, basi na maendeleo ni rahisi kupatikana. Wakulima wadogo wamekosa mbinu zinazoweza kuwawezesha kufika mbali lakini hiyo haimaanishi kuwa wamechelewa. Ili kuweza kufanya mabadiliko katika kilimo, lazima mkulima achukue hatua na kuzingatia mbinu zifuatazo ili kuchochea uzalishaji.

Vikundi

Siku zote huwa wanasema kuwa umoja na ushirikiano huleta mafanikio zaidi. Hii inaweza kutumika kwa wakulima pia hasa wadogo. Kwasababu wengi wao huwa hawana uwezo wa kufanya kilimo kikubwa au kutumia vifaa vya kisasa kuzalisha mazao zaidi. Basi wanashauriwa kuungana kwa pamoja kwa kuunda vikundi baina yao na kupitia vikundi hivyo wanaweza kuchangiana kiasi cha fedha kwa kipindi cha muda fulani ili waweze kufanya mabadiliko kwamfano, badala ya kulima na ng’ombe wanaweza kukodi trekta ambalo litalima katika mashamba yote ya wanakikundi kwa muda mfupi, badala ya kutumia mbolea za asilia kupitia fedha walizochanga na mipango wanaweza kununua mbolea za kisasa ambazo zina uhakika wa kuongeza uzalishaji hivyo pale faida katika mazao inapopatikana wanakuwa na uwezo wa kuboresha mambo mengine katika kikundi husika kwa lengo la kupata maendeleo zaidi kwamfano kukata bima ya mazao n.k.

ADVERTISEMENT

Masoko

Wakulima hasa wadogo wakitafuta au kutafutiwa masoko itawahamasisha kuzalisha zaidi ili kukidhi mahitaji ya soko. Wizara ya Kilimo imekuwa ikifanya kila jitihada kuwatafutia masoko wakulima hasa wadogo nje ya nchi ili wazidi kuzalisha mazao husika na pia waweze kujipatia maendeleo binafsi na kuchangia katika pato la taifa. Kwa mfano, serikali ilipoona wakulima wanapata shida kuhusu masoko ya zao la korosho, waliamua kutafuta suluhisho ili wakulima wa zao hilo wasikate tamaa na waendelee kuzalisha.

Elimu

Ni muhimu sana kwa wakulima hasa wadogo kujipatia elimu kwa wataalamu waliobobea katika masuala ya kilimo. Ili kwanza kuwaondolea hofu kuhusiana na kilimo cha kisasa na vifaa vyake, pili kuwahamasisha kufanya mambo mapya na si kwa mazoea hii itasaidia kuimarisha uzalishaji kwa sababu kukosa elimu hususani ya mambo muhimu kama teknolojia ndio sababu mojawapo inayowafanya waendelee kuzalisha mazao kidogo. Hivyo basi wanaweza kupewa elimu kwa makundi, na wataalamu wanaweza kwenda katika mashamba ya kila mkulima kujionea hali halisi na kutoa ushauri zaidi.

Endapo wakulima watakuwa na utayari kuendeleza sekta ya kilimo, itakuwa rahisi kusonga mbele na kuleta maendeleo.

About Us

PesaTu ni kitengo cha habari cha MediaPix ambacho huandika makala za biashara na uchumi wa Tanzania na Afrika Mashariki kwa ujumla. Waasisi wa kampuni wana uzoefu mkubwa kwenye tasnia ya habari na mawasiliano wakiwa kwenye fani hio tangu mwaka 1905.

Editors' Picks

Newsletter