Wakulima wa zao la mwani wametakiwa kuwa wavumilivu wakati serikali ikitafuta suluhisho la bei ya zao hilo visiwani Zanzibar. Hayo yamesemwa na Rais wa Zanzibar Dk. Ali Mohamed Shein katika ziara yake wilaya ya kusini mwa Unguja. Dk. Shein amesema amekuwa akifuatilia kwa ukaribu sana suala la bei ya zao hilo ambalo ni changamoto kubwa kwa wakulima hao na hadi sasa wako katika hatua za mwisho za kutatua tatizo hilo.
Rais Shein amesema serikali imekuwa ikifanya majadiliano na kampuni kubwa ya mwani iliyopo nchini Indonesia na wameshakubali kujenga kiwanda cha zao hilo Zanzibar, ikiwa ni hatua mojawapo ya kuongeza thamani ya zao hilo.
Pia ameongeza kuwa kufuatia ziara zake hapo mwaka jana, ameweza kuwahamasisha wakulima hao kuunda umoja ambao utawafanya wanufaike zaidi na hadi sasa kilichobakia ni kusaini mkataba kati ya serikali na kampuni hiyo mradi huo uanze kutekelezwa. Uwepo wa kiwanda hicho utasaidia bei kuwa juu na wakulima hao kupata faida na hivyo kukuza uchumi na pato la taifa.