Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Angellah Kairuki amesema serikali itaendeleza jitihada za kujenga mazingira rafiki na endelevu katika sekta ya kilimo kupitia sera imara na zinazotekelezeka. Kairuki ameeleza hayo jijini Dodoma wakati akifungua kongamano la tano la wadau wa sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhusu sera, kwa niaba ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Kairuki amesema kuwa lengo hilo la serikali linaenda sambamba na mchango wa sekta ya kilimo katika uzalishaji na ukuaji wa uchumi kwa kuzingatia namna kilimo kinavyochangia katika maeneo mbalimbali ikiwemo ajira kwa wananchi.
“Ni mambo ambayo yanajieleza yenyewe na kila mmoja wetu anayajua vizuri. Asilimia 65.5 ya watanzania wanategemea ajira na maisha yao kwenye kilimo, pia kinachangia asilimia 95 ya mahitaji ya chakula nchini na asilimia 65 ya malighafi ya viwanda vyetu”. Amesema Waziri Kairuki
Pamoja na jitihada mbalimbali zinazofanywa na serikali, Waziri huyo pia ametaja baadhi ya changamoto katika sekta hiyo ikiwemo utegemezi wa jembe la mkono, matumizi madogo ya mbegu bora na kilimo kutegemea mvua kwa kiasi kikubwa pasipo kuwekeza katika kilimo cha uhakika cha umwagiliaji.